Rai imetolewa kwa mabaraza ya kata katika Wilaya ya Hai kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia misingi na maadili ya kazi zao na kujitenga na vitendo vinavoashiria rushwa wakati wa kushughulikia migogoro inayofikishwa kwao.
Rai hiyo imetolewa na mwanasheria wa wilaya ya Hai Blandina Mweta wakati wa mafunzo ya muongozo wa uendeshaji wa mabaraza ya kata yaliyofanyika katika Kata ya Bondeni.
Kauli hiyo imefuatia shutuma nyingi kutoka kwa wananchi kuwa wajumbe wa mabaraza ya kata wanajihusisha na matukio yanayoashiria kupokea rushwa na kufanya maamuzi kwa upendeleo kwa sababu ya ushawishi.
Pia ameendelea kusisitiza kuwa wananchi wanatoa shutuma hizo bila uthibitisho na kuwasihi wale wote watakaoshindwa kesi na kuona wameonewa wakate rufaa katika mahakama ya baraza za ardhi ya wilaya au mahakama ya mwanzo na sio kulalamika.
Mweta amewakumbusha wananchi kuwa iwapo kuna mtu atakuwa na ushahidi wa tuhuma za vitendo vya rushwa anapaswa kupeleka malalamiko yake katika mamlaka zinazohusika na mapambano ya rushwa.
Na ameendelea kuwasisitiza wajumbe wa baraza la kata watende haki katika kutimiza majukumu yao na kutafuta suluhu kabla ya kusikiliza kesi.
Kwa upande wake Afisa wa TAKUKURU kituo cha Hai Julius Msoka amewakumbusha wajumbe wa mabaraza ya kata kuepuka vitendo vinavyoashiria mazingira ya rushwa kama kupokea hongo au zawadi mbalimbali kutoka kwa mtu mwenye kesi.
Matukio mengine yanayotakiwa kuepukwa ni pamoja na ushawishi wa kingono na watu wanayemhudumia kwenye baraza hilo akiwa ni mlalamikaji au mlalamikiwa kitu ambacho kitaathiri maamuzi ya shauri husika.
Aidha Msoka amesema moja ya majukumu ya TAKUKURU ni kuzuia rushwa kwa kutoa elimu na namna ya kutambua na kuepuka vitendo vya rushwa kwenye mazingira tofauti.
‘’Tunatoa elimu kwa wananchi, wa rika na kazi mbalimbali ikiwemo wajumbe wa mabaraza ya kata ili waweze kuelewa dhana ya rushwa na madhara yake ili waweze kutuunga mkono katika mapambano hayo”
Mafunzo kwa wajumbe wa mabaraza ya kata ni namna ya kuwaongezea uwezo katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi huku wakizingatia sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo kuepuka vitendo vya rushwa ili kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai