Wito umetolewa kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro hususani wakulima kujitokeza kununua matrekta kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo.
Wito huo umetolewa hii leo na Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa katika hafla ya kukabidhi tela la trekta na michoro yake iliyofanyika katika kiwanda cha Machine Tools Machame wilayani Hai.
Amesema kuwa katika kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati wakulima wanayo nafasi kubwa kuipeleka nchi katika ujenzi wa viwanda ikiwa ni kwa sababu idadi kubwa ya watanzania ni wakulima na kwamba malighafi nyingi za viwanda zinatokana na kilimo.
Aidha amewataka KMTC kwa kushirikiana na SIDO kujikita kuwasaidia wakulima wadogo kwa kutengeneza zana ndogondogo za kilimo kwa ajili ya matumizi ya shambani.
Pia ameelekeza NDC kwa kushirikiana na TEMDO, KMTC na SIDO kuandaa mpango mkakati wa namna ya kushughulikia changamoto za viwanda nchini.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira amewataka wasimamizi wa kiwanda hicho kuweka nguvu kwenye uzalishaji ili kukuwezesha kiwanda kukidhi mahitaji ya uendeshaji ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi, huduma za umeme na maji pamoja na mahitaji mengine lakini pia kufanya kazi kwa bidii kurudisha hadhi na heshima ya kiwanda hicho kilichokuwa kinafanya kazi usiku na mchana na kuajiri watu wengi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amewashauri MDC kutumia ardhi iliyopo kwa kushirikiana wawekezaji wengine ikiwemo sekta binafsi ili kutumia kikamilifu ardhi iliyopo yenye zaidi ya ekari 500 hasa ikizingatiwa eneo hilo kuwa muhimu kwa uwekezaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo ameahidi kutoa ushirikiano kwa kutumia redio ya halmashauri yake (Radio Boma Hai FM) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na kiwanda hicho.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Hai Kumotola Kumotola ameshauri kupewa kipaumbele wananchi wa wilaya ya Hai na maeneo ya karibu katika kupata ajira kwenye kiwanda hicho ili kuifanya jamii inayozunguka kuwa sehemu ya kiwanda hicho.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai