Mkuu wa polisi wilaya ya Hai Mrakibu Mwandamizi wa jeshi la Polisi SSP Juma Majatta ametoa onyo kwa baadhi ya madereva ikiwemo waendesha bodaboda na bajaji kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwa ni pamoja na kushiriki kubeba mali za wizi.
Majatta ametoa onyo hilo leo Juni 20, 2022 wakati akifungua mafunzo maalumu ya usalama barabarani yanayofanyika katika ukumbi wa Polisi wilayani Hai yanayoendeshwa na chuo cha udereva Winners, nakueleza kuwa wapo baadhi ya vijana wanaoendesha bodaboda na bajaji hawana leseni wala vyeti na bado ni wahalifu.
Aidha amewatahadharisha baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutokuingia kwenye mitego ya kusafirisha mali za wizi kwani atakayebainika atafikishwa kwenye vyombo vya dola.
“Huna cheti huna leseni na bado ni mhalifu,nawaomba baada ya mafunzo haya msiwe sehemu ya wahalifu na mara nyingi wahalifu wanawatumia vijana wa bodaboda na bajaji, mnatumika vibaya wakati mwingine mnajua na wakati mwingine hamjui”
Kwa upande wake mtaalamu kutoka chuo cha udereva Winners Medard Kiheka ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa watumiaji wote wa barabara huku wakiwalenga zaidi wale wanaotakiwa kuwa na leseni za udereva kwa mujibu wa sheria.
Kiheka amebainisha kuwa 80% ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu hali iliyopelekea wao kuwekeza nguvu kwenye elimu kwa lengo la kupunguza visababishi vya ajali za barabarani zinazosababishwa na uzembe wa baadhi ya madereva wa vyombo vya moto.
“Tumeamua kuwekeza nguvu kwenye elimu lengo ni kuweza kupunguza hizi 80% ambazo zinapelekewa na makosa ya binadamu,ambapo pia tunaweza kuyamaliza kupitia elimu”
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai