Madiwani Waishukuru Serikali Miradi ya Maendeleo Hai
Imetumwa: July 29th, 2021
Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha zinapelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo.
Wakizungumza kwa niaba ya madiwani wengine; Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Evod Njau amesema anaishukuru Serikali kwa fedha zinazoletwa kutekeleza miradi inayosaidia kuimarisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Hai.
Njau amesema hayo baada ya ziara ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya halmashauri hiyo kutembelea na kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.
Amesema wametembelea ujenzi wa Zahanati ya Chemka, Ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Zahanati ya Kwatito, ujenzi wa matundu ya choo kwenye shule za Msingi Shirimgungani, Bomani na Kengereka.
Miradi mingine ni ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule za Msingi Uhuru, Kengereka na Bomani kupitia mradi wa lipa kwa matokeo (EP4R).
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Lyamungo Hausen Nkya amewapongeza walimu wakuu wa shule zinazotekeleza miradi hasa walimu wanawake kwa umakini wao katika kusimamia fedha za miradi.
Aidha amewahamasisha wananachi kushiriki katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao kwa kuchangia nguvu kazi na utaalamu ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali.
Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa matundu 12 ya vyoo Shule ya Msingi Bomani kwa Shilingi 13,200,000, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa Shule ya Msingi Uhuru kwa Shilingi 40,000,000; ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa, matundu 12 ya vyoo katika Shule ya Msingi Kengereka kwa Shilingi 65,701,908.