Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utunzaji wa mazingira ikiwemo kuzuia ukataji holela wa miti unaosababisha mabadiliko makubwa ya tabia nchi.
Rutaraka ambaye ni diwani wa kata ya Muungano wilayani humo amesema kuwa licha ya kwamba mchakato wa vibali vya ukataji miti vinapitia kuanzia ngazi ya vijiji hadi wilayani lakini pia madiwani wanayo nafasi ya kusimama imara kuhakikisha ukataji wa miti kiholela unadhibitiwa.
Ameyasema hayo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo kufuatia hoja iliyoibuliwa na diwani wa kata ya Mnadani Nasibu Mndeme ya kuweka msisitizo wa namna ya kusimamia utunzaji wa mazingira katika wilaya ya Hai.
"Hoja hii pamoja na kuletwa kwenye baraza letu, lakini tayari Mhe. Mkuu wa wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya tayari alishaanza kulishughulikia, kwahiyo sisi kwenye baraza tulileta ili kuweka msisitizo na madiwani wote waweze kuwa na lugha moja ya kuhakikisha wanasimamia mazingira"
Kwa upande wake katibu Tawala wilaya ya Hai Upendo Wella amewataka viongozi wa ngazi za chini wakiwemo watendaji na madiwani kuhakikisha wanachukua hatua za kuzuia uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti usiofuata taratibu.
Naye mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dionis Myinga ameeleza kuwa jukumu la kutunza mazingira ni la kila mtu na kuwataka wananchi wote wa wilaya hiyo kushirikiana katika kutunza mazingira.
Katika hatua nyingine baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Hai limeunda kamati ndogo yenye wajumbe wanne ambayo imepewa mwezi mmoja kuchunguza vitendo vya uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji wilayani humo baada ya kusemekana kuwa kuna watu wamekuwa wakivamia na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kwenye vyanzo vya maji.
Wajumbe walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni diwani wa kata ya Mnadani Nasibu Mndeme, diwani wa kata ya Masama Magharibi Machoya Natai, pamoja na madiwani wa viti maalum Ausen Nkya na Upendo Sawe.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai