Watumishi wa mahakama katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamehimizwa kuendelea kuzingatia kanuni na miongozo ili kuisaidia mahakama kufanya kazi ya utoaji haki kwa weledi na kwa kuzingatia sheria.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauria ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo wakati akimuakilisha mkuu wa wilaya hiyo katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria wilayani humo inayoenda sambamba na miaka 100 ya mahakama kuu iliyoanza leo kwenye viwanja vya mahakama ya mwanzo mjini Bomang’ombe.
Amesema kuwa endapo watazingatia miongozo na kanunu basi mahakama itaendelea kutoa haki na kuisaidia nchi kustawi na kuendelea kuwa huru zaidi huku akiwataka kumtanguliza Mungu katika kazi wanazozifanya na kuwatendea wananchi haki.
Pia ametoa wito kwa wananchi kufika katika viwanja vya mahakama hiyo kupata ushauri na msaada wa kisheria bila malipo na kwamba miongoni mwa elimu itakayotolewa viwanjani hapo ni pamoja na taratibu za ufuanguaji wa mashauri, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, ndoa na talaka, utekelezaji wa hukumu, sheria za watoto na taratibu za mashauri ya mirathi na mambo mengine.
Wananchi watakaofika watapata fursa ya kusikilizwa na jopo la majaji, wasajili, manaibu wasajili, mahakimu pamoja na wadau wa mahakama.
Aidha, Sintoo ametumia nafasi hiyo kuipongeza Mahaka Kuu ya Tanzania kwa kuadhimisha miaka 100 (karne moja) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1921 huku akiwashauri kutafakari kwa kina mambo yanayotakiwa kuboreshwa ili kuendelea kudumisha amani, uhuru, udugu na haki kwaajili ya ustawi wa nchi yetu.
Kwa upande wake hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Hai Mhe. Julieth Mawole amesema maadhimisho hayo yameanza rasmi leo Jumapili na yatafikia tamati Januari 29 hivyo amewahimiza wakazi wa Hai kujitokeza kwa wingi kutembelea viwanja vya Mahakama ya Mwanzo ili kupata elimu ya masuala yanayohusu mahakama na mwenendo wa mashauri.