Makabidhiano Wakurugenzi: Sintoo AShukuru Ushirikiano Halmashauri ya Hai
Imetumwa: August 9th, 2021
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai anayemaliza muda wake Yohana Sintoo anajivunia mafanikio ya Halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano aliyokuwa msimamizi wa shughuli za maendeleo.
Sintoo amezungumzia Halmashauri ya Wilaya kupata hati safi kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2021 anapoikabidhi kwa Mkurugenzi mwingine.
Pia amesema Halmashauri imefanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo ya muhimu kwa wananchi katika sekta za elimu, afya, kusambaza maji na huduma nyingine za msingi kwa ustawi wa wananchi.
Aidha Sintoo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo; waheshimiwa Madiwani pamoja na watumishi wote wa Halmashauri ya Hai kwa ushirikiano waliompatia wakati wote alipokuwa Mkurugenzi wa Wilaya hiyo.
Amebainisha hayo wakati akikabidhi ofisi ya Mkurugenzi kwa Dionis Myinga aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupokea jukumu hilo katika uteuzi uliofanyika hivi karibuni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga amesema yupo tayari kufanya kazi katika Halmashauri ya Hai kutekeleza majukumu yanayompasa kwa nafasi yake akitumia uwezo na taaluma yake kufanikisha majukumu yake.
“Mimi kwenye kazi siyo mgeni, nimekuwa Mkurugenzi huko nilikotoka, nafahamu namna ya kufanya kazi kwa utaratibu”
“Pia nitafanya ziara ya kuzungukia miradi iliyotekelezwa na ile inayoendelea kutekelezwa kwenye halmashauri ili nipate kwa kuanzia katika kutekeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na mtangulizi wangu” Amesisitiza Myinga.
Amebainisha kuwa kwa kushirikiana na madiwani na watumishi kwa pamoja watashirikiana kuwaletea wananchi maendeleo wanayohitaji.
Aidha amemshukuru mtangulizi wake Yohana Sintoo kwa kazi nzuri alizozifanya ambazo matokeo yanaonekana kwa kubadilisha miundombinu na maisha ya wananchi kwenye halmashauri.
Zoezi la makabidhiano ya ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai limefanyika mbele ya Wakuu wa Idara na Vitengo likisimamiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Muungano Edmund Rutaraka.