Mamlaka zinazojuhusisha na huduma ya maji kwa jamii imetakiwa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria ya Maji namba 12 ya mwaka 2009 inayoeleza wazi namna ya kushirikiana kati ya wahusika wakuu wa huduma hiyo ikiwemo serikali na vyombo vingine.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Emmanuel Kalobelo ametoa agizo hilo kama mwongozo wa namna ya kushughulikia mambo yanayohusu huduma ya maji kwenye ngazi ya wilaya na mkoa ikiwemo kufahamu majukumu na mipaka ya wadau hao wakuu wa sekta ya maji.
Akizungumza na wadau wa huduma ya maji safi na maji taka katika wilaya za Hai na Siha alipofanya ziara ya kikazi kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na wizara hiyo, amesema vyombo vinavyotoa huduma ya maji vinatakiwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa na kusimamia lengo kuu la kuwapatia huduma bora wananchi hasa kwa wakati huu ambapo nchi inapita kwenye mageuzi ya uchumi.
Kalobelo ameziagiza bodi za maji kuhakikisha kuwa gharama za kuvuta maji nyumbani zinakuwa nafuu ili kila mwananchi aweze kuzimudu ili kuweza kufikia malengo ya taifa la upatikanaji wa maji kwa jamii.
Amefafanua kuwa lengo la kuanzishwa kwa mamlaka za utoaji wa huduma za maji ni kuisaidia serikali kufanikisha usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi kwa mujibu wa sheria ya maji.
“Bodi za maji zitaendesha shughuli zake kwa kufuata sheria za nchi na ili kuweza kutoa huduma za maji ni lazima usajiliwe kwenye mamlaka zinazohusika ili kuweza kupata eneo la kutolea huduma ya maji kwa jamii ya eneo husika ”alisema Mhandisi Kalobelo
Aidha, Mhandisi Kalobelo alibainisha kuwa bodi za maji zitasaidiana na serikali kuboresha miundombinu pamoja na kuhakikisha kuwa zinafungua milango yake kwa wakaguzi wa serikali ili kuweka uwazi wa namna bodi hizo zinavyojiendesha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo amesema kuwa amepokea agizo la Wizara la kuweka uelewa wa pamoja na kuhakikisha sheria za maji zinafuatwa na huduma za maji zinaboreshwa kwa manufaa ya wananchi wote.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Verial Juwal amesema kuwa wilaya hiyo ina bodi tatu zinazohudumia wakazi zaidi 120,000 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 kwenye kata 17 za wilaya ambapo kwa sasa wananchi wanapata maji kwa asilimia 84.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Bodi ya Lyamungo-Umbwe Michael Mmasy amesema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha kuwa huduma za maji zinaboreshwa kwa kuwafikia wananchi wote wanaofikiwa na mtandao wa maji .
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai