Mwenge wa Uhuru umeendelea kufanikisha jukumu la kuangaza Tanzania ikiwa ni pamoja na kuamsha kiu ya maendeleo kwa wananchi wa maeneo unapopita.
Katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Mwenge wa Uhuru umefanikisha hilo kwa kuchangia ukarabati wa majengo ya shule ya Msingi Kibohehe ambayo iliezuliwa paa.
Akielezea tukio hilo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2018, Mkuu wa wilaya ya Hai Nengai Ole Sabaya amesema wamekusanya michango kutoka kwa wadau, watumishi wa umma na wananchi kugharamia shughuli za mwenge na kupata zaidi shilingi milioni 34 na kutumia milioni 30 na laki 9.
Amesema uongozi wa Wilaya umeamua kutumia fedha zilizobaki kununua mifuko 138 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni mbili huku kiasi cha shilingi milioni mbili kikikabidhiwa kwa ajili ya kufanikisha lengo la kuirudisha shule hiyo kwenye hali bora ili wanafunzi waweze kusoma bila bugudha.
Akikabidhi mchango huo wa saruji na fedha taslimu Kiongozi wa Mbio za Mwenge Charles Kabeho ameipongeza wilaya ya Hai na watu wake kwa kutekeleza kwa vitendo dhana ya kuwekeza kwenye elimu kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu inayohamasisha jamii kuwekeza kwenye elimu kwa maendeleo ya Taifa.
“Nachukua nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Wilaya ya Hai kwa kufanya maamuzi sahihi ya kimaendeleo lakini pia wananchi kwa kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo” Amesema Kabeho.
“Niwaombe ndugu wananchi muendelee kuchangia maendeleo kwa michango ya fedha taslimu, vifaa au nguvukazi ili kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma” ameongeza Kabeho.
Aidha Kabeho ameipongeza Wilaya ya Hai kwa kushiriki kikamilifu kwenye Mbio za Mwenge mwaka 2018.
“Wakati wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru Wilayani Hai tumefarijika sana kuona namna wananchi walivyojitokeza kuulaki kwenye maeneo ya miradi na maeneo yote Mwenge wa Uhuru ulipopita”
Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 umekimbizwa kwenye jumla ya kilometa 98 katika Wilaya ya Hai na kutembelea miradi ya maendeleo ambayo miradi miwili imezinduliwa na mmoja umewekewa jiwe la msingi yenye thamani ya shilingi milioni 461,649,943.
Miradi hiyo iligusa sekta ya kilimo kwa kuzindua shughuli za kuzindika zao la vanilla, uzinduzi wa duka la dawa katika hospitali ya Wilaya ya Hai pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa ukuta wa uzio wa shule ya sekondari ya wasichana ya Machame.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai