Mbunge Hai Achochea Maendeleo Kutumia Mfuko wa Jimbo
Imetumwa: April 4th, 2021
Mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro Saashisha Mafuwe amekabidhi mchango wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 10 katika shule ya sekondari Mailisita kuwezesha ujenzi wa vyumba vitatu (3) vya madarasa.
Mafuwe amekabidhi vifaa hivyo jana April 3, 2021 alipofanya ziara maeneo mbalimbali ya jimbo la Hai na kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya jimbo hilo.
Vifaa vilivyokabidhiwa katika shule hiyo ni saruji mifuko 132, mawe, nondo, kokoto na mchanga ambapo mbunge huyo amemtaka Afisa Elimu kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika katika malengo yaliyokusudiwa huku akiahidi kurejea shuleni hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa hayo.
"Ninachotegemea vifaa hivi vikatumike kadri ya matarajio yetu ujenzi unaofanyika ukafanyike kwa kutumia force account"
"Mimi nitarejea tena kuja kukagua niombe ujenzi usimamiwe vizuri na mhandisi wa wilaya na madarasa yanyooke" amesema Mafuwe.
Aidha Mafuwe ameiomba serikali kujenga bweni katika shule hiyo kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa Elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo kwani baadhi yao wamekuwa wakitokea vijiji vya mbali hali inayowalazimu kutembea umbali mrefu zaidi ya kilometa 8.
Kwa upande wake Afisa Elimu wilaya ya Hai Julius Mduma akizungumzia hali ya miundombinu ya shule katika wilaya hiyo ameeleza kuwa mkakati uliopo kwa sasa ni kuhamasisha wananchi kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya maabara ili kuwapatia wanafunzi fursa ya kusoma kikamilifu masomo ya sayansi.
Naye makamu mkuu wa shule ya sekondari Mailisita Nicodemas Alexander amebainisha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 627 inaupungufu wa matundu 19 ya vyoo ambapo kwa sasa matundu yaliyopo ni 7 pekee na kumwomba mbunge huyo kuangalia namna ya kuwasaidia kwenye mkakati wao wa kuongeza matundu hayo.
Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe pamoja na kutumia ziara hiyo kukabidhi vifaa vya ujenzi katika shule ya sekondari Mailisita, pia amekabidhi vifaa vingine katika chanzo cha mfereji wa maji eneo la msikitini vyenye thamani ya shilingi milioni 5.2 kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo.