Mbunge wa Hai Akabidhi Vifaa Tiba Zahanati ya Kware
Imetumwa: January 9th, 2021
Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe amekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili katika Zahanati ya Kware iliyopo Kata ya Masama Kusini katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.
Mafuwe amesema amekabidhi vifaa hivyo ni kupunguza changamoto zilizopo katika Zahanati hiyo ambayo imekuwa ikitumiwa na wananchi kupata huduma za afya.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji wa cha Kware, leo Januari 9,2021 mbunge huyo amesema kuwa msaada wa vifaa hivyo ambavyo ni mashine za kupimia wingi wa damu hasa kwa wanawake wajawazito pamoja na kifaa cha kupimia sukari ni moja ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni.
"Ndugu zangu leo nimekuja katika Zahanati hii kukabidhi vifaa hivi muhimu ili kusaidia ndugu zetu wanaofika katika Zahanati hii kupatiwa matibabu mbalimbali, kwa hiyo vifaa hivi vitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizopo hapa," Amesema Mafuwe.
"Mnakumbuka mwaka jana niliwaahidi kuwa endapo mkinichagua nitarudi hapa, nashukuruni kwa kunichagua ndio maana nimerudi hapa, nimeamua kutoa msaada huu wa vifaa tiba vyenye thamani ya milioni mbili kusaidia Zahanati hii na hii ni moja ya ahadi zangu nilizozitoa wakati wa kampeni," Ameongeza.
Mbunge huyo amekuwa na utaratibu wa kukutana na wananchi wa jimbo lake kwenye mikutano ya hadhara kwenye kata na vijiji kwa lengo la kuwashukuru kwa kumchagua pamoja na kusikiliza changamoto walizonazo na kujadili namna ya kuzitatua.