Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ameagiza wenyeviti wa vitongoji, vijiji na watendaji kijiji na kata kutopokea fedha zozote zinazotokana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo yao badala yake watoe taarifa ya migogoro hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji na ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Sanya Station kata ya Kia Wilayani Hai, Sabaya amesema serikali haiwezi kuvumilia kuona migogoro hiyo ikiendelea na kuwaasa watendaji na wenyeviti kuepuka kuwa sehemu ya mgogoro kutasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza migogoro hiyo.
“Kwa namna yoyote ile serikali haitavumilia unyanyasaji wowote utakaofanywa kwa wafugaji wala haitavumilia kuona wafugaji wanaonea wakulima, hivyo ni marufuku kwa wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kila mkulima abaki katika eneo lake ili kuepuka migogoro.“ Alisisitiza Sabaya.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka jamii ya wafugaji kufuga kibiashara kwa kuwa na mifugo michache yenye afya nzuri na kutii sheria za nchi ili kuzua migogoro baina yao na wakulima
Amesema serikali ya awamu ya tano inawathamini na kuwapenda wafugaji kwa kuwa wana haki sawa na wakulima na wafanyakazi hivyo nao wanao wajibu wa kutii mamlaka na sheria zilizopo.
Amesema wizara yake inatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo ibara ya 25 kifungu a hadi q inawazungumzia wafugaji na kuwaondoa hofu iliyopo miongoni mwao ya kwamba serikali haiwathamini.
“Mhe. Waziri Mpina amenituma niwaambie na niwahakikishie wananchi wa Hai hasa wafugaji kuwa Rais John Magufuli ni kipenzi cha wafugaji, hivyo amewataka mmtunzie heshima hiyo na mjue kuwa serikali inatambua haki ya wafugaji na mtembee kifua mbele” amesema Prof. Gabriel.
Amesema kuwa mifugo haiwezi kuendelezwa bila ya kuwaendeleza wafugaji kwa kua vyote vinategemeana na kwamba wizara inaendelea kuboresha na kufanyia kazi changamoto za wafugaji kwa kuwa mifugo inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi akitolea mfano wa ng’ombe na mazao yake ambayo imeajiri kundi kubwa la wananchi.
Naye Katibu wa wafugaji nchini Magembe Mkaoye ameiomba serikali kuweka mpango wa matumizi bora ili kutenga eneo la kulishia mifugo na eneo la wakulima ili kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Ameongeza kuwa wafugaji wanategemea mifugo katika kukidhi mahitaji yao ya kifamilia pamoja na uchumi wao hivyo ameasa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji kuheshimiwa ili kuepuka changamoto ambazo zinaarudisha nyuma maendeleo.
Kwa upande wao wananchi waliopata nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wenzao wameiomba serikali kuwatengea maeneo rasmi ya malisho na kuwajengea majosho ya mifugo na kuwapa elimu ya kuhudumia mifugo na kutambua magonjwa yanayowasumbua, maombi ambayo katibu Mkuu alihidi yatafanyiwa kazi mapema.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Hai akiwa na lengo kuu la kufahamu changamoto zinazowakabili wafugaji ikiwa ni hatua ya kuimarisha shughuli za ufugaji nchini.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai