“Serikali kuwahimiza mjiunge kwenye vikundi ili kuweza kupatiwa mikopo ni namna ya kuwaweka pamoja watu wenye ujuzi na uzoefu tofauti utakaosaidia kuwainua kiuchumi kwa kutumia maarifa tofauti yaliyopo kwenye kikundi”
Hayo ni maneno ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo wakati akifungua mafunzo kwa vikundi kuhusu namna ya kutumia kwa tija mikopo inayotolewa na serikali.
Sintoo amesema kuwa mikopo hiyo inayotolewa na serikali kupitia makusanyo ya halmashauri ipo na inawahusu wananchi wote ambao wapo tayari kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali pamoja na kukidhi masharti na taratibu za kuweza kupatiwa mkopo.
“Serikali inaamini kuwa watu wote wao uwezo wa kufanya kazi za kujiingizia kipato lakini wapo watu wanoshindwa kutimiza hilo kwa kukosa mtaji; mikopo hii inalo lengo kuu la kuinua hali ya kiuchumi ya kila mwananchi kwa kuwapa fursa ya kujitengenezea kipato halali”. Amesisitiza Sintoo.
Awali akizungungumza wakati wa kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji; Afisa Maendeleo ya Jamii Lucas Msele amesema kuwa mikopo hiyo hutolewa kwa vikundi ambavyo tayari vimeshatembelewa na kufanyiwa tathmini na kuona kuwa wanastahili kupewa mikopo, wanaelekezwa namna ya kufanya marejesho, elimu ya ujasiriamali pamoja na elimu ya kuweka na kukopa.
Msele amesema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Raisi Dr. John Magufuli imeondoa riba kwa vikundi vyote vinapochukua mkopo kutoka Halmashauri lengo likiwa ni kuwaondolea umasikini watanzania hasa wanawake, vijana na walemavu.
Pia Msele amewapongeza watumishi wa idara ya maendeleo ya jamii, watendaji kata na viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana kwa pamoja kusimamia vikundi na kuhakikisha vile vinavyokidhi vigezo ndivyo vinavyopatiwa mkopo ili viweze kuzalisha na kurejesha mikopo hiyo.
Kwa upande wao wanavikundi waliopata mikopo kutoka halmashauri ya wilaya ya Hai wameishukuru serikali kwa kuwapatia mkopo usiokuwa na riba na kusema kuwa wamefurahishwa na hatua hiyo na kwamba shughuli za vikundi hivyo zitafanyika kwa ufanisi baada ya mkopo huo usiokuwa na riba.
Katibu wa kikundi cha AGROP kutoka kijiji cha KwaSadala wilayani hapa Clara Njigilile amesema kikundi chake kinashukuru kupatiwa mkopo huo usio na riba na kuahidi kurejesha mkopo huo mapema ili kuwapa nafasi wananchi wengine waweze kukopa.
Naye mwakilishi wa kikundi cha walemavu wa ngozi kutoka kata ya Muungano amesema mafunzo ya jinsi ya kutumia na kurejesha mkopo kutoka halmashauri yamewasaidia kuwa na uelewa na watayafanyia kazi katika kupata faida kubwa na kurejesha mkopo huo.
Aidha Vikundi saba vya wanawake, kimoja cha watu wenye ulemavu na vikundi vitatu vya vijana vimenufaika na mkopo huo wa shilingi 25,600,000 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Hai ili kuwaongezea wananchi husika uwezo wa kujiongezea kipato na kureshesha fedha hizo bila riba ili ziweze kuwasaidia wengine kuinuka kiuchumi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai