Mila potofu, ushirikiano hafifu vimetajwa kuchangia vitendo vya ukatili hususani kwa watoto kuendelea kushika kasi kwenye jamii na kurudisha nyuma juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Akizungumza kwenye kikao cha Afya ya Msingi wilaya ya Hai kilichoketi kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo, mkuu wa wilaya ya Hai Juma Irando ameonyesha kushangazwa na baadhi ya jamii kuendelea kukumbatia mila zilizopitwa na wakati ikiwemo kutumia jani la sale kuomba msamaha na kumaliza vitendo vya ukatili vinapotokea, hali ambayo inamnyima haki mhanga wa tukio.
"Kwahiyo akishabeba tu hilo jani ni basi? hata kama ameua? Wananchi waendelee kuhamasishwa na kuelimishwa, wapewe elimu kwamba waachane na mila potofu, tuziepuke mila ambazo zinaonekana kuwa ni changamoto, twende na wakati" Irando
Aidha mkuu huyo wa wilaya ameitaka jamii ikiwa ni pamoja na jamii ya kifugaji kuachana na mila na desturi potofu ikiwemo kuozesha watoto wadogo kwa nia ya kupata mahari kwani kufanya hivyo ni ukatili na unaokatisha malengo ya mtoto.
Kwa upande wake Katibu Tawala wilaya ya Hai Upendo Wella akizungumza kwenye kikao hicho, ameitaka jamii kuchukua hatua madhubuti za kukataa na kukomesha vitendo vya ukatili hususani kwa watoto na watu wengine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga amesisitiza kila mmoja kuendelea kuzuaia na kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto na watu wote walioko kwenye hatari ya kufanyiwa vitendo hivyo.
Awali akiwasilisha taarifa ya ulinzi na usalama wa mtoto, Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Hai Salome Zefania ametaja sababu za matukio ya ukatili kuongezeka, moja wapo ikiwa ni matumizi makubwa ya mila na desturi ikiwemo majani ya masale katika kusameheana vitendo vya ukatili na kuvimalizia nyumbani "hata aliyetoa taarifa ya ukatili, siku ya kutoa ushahidi hatokei mahakamani"
Naye mganga mkuu wa wilaya ya Hai Dkt. Itikija Msuya amesema wamejipanga kuendelea kutoa elimu ili kukabili vitendo vya ukatili kwani baadhi ya watu wanaofanya ukatili huo hasa kwa watoto, huwatishia kuwa watawaua na watoto wakitishiwa siyo rahisi kutoa siri kwa kuhofia maisha yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Edmund Rutaraka akizungumza katika kikao hicho amesisitiza usimamizi thabiti ikiwa ni pamoja na uwazi wa fedha zinazotolewa na Serikali kwenye miundombinu ya afya na kuongeza kuwa wamepokea takribani bilioni 1.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Afya.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai