Zaidi ya shilingi milioni sabini na saba zimetolewa kwa vikundi 14 vya wajasiriamali wadogo katika halmashauri ya wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.
Akikabidhi hundi hiyo leo kwa vikundi hivyo katika ukumbi wa Halmashauri ya Hai, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Upendo Wella amevitaka vikundi kutumia fedha hizo kwa uaminifu na kuhakikisha zinazalisha kwa faida ya Taifa na faida yao binafsi.
Amesema fedha wanazokopeshwa zinarudishwa bila ya Riba hivyo ni wakati wao kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira kwa watanzania wengine.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai, Wang’uba Maganda ameishauri halmashauri hiyo kuona uwezekano wa kuwakopesha wananchi mikopo mikubwa yenye tija zaidi ili kujihusisha na miradi mikubwa itakayozalisha ajira nyingi.
Aidha Maganda amewaasa wananchi waliopata mikopo hiyo kupeleka fedha walizopata kwenye miradi waliyoombea mkopo na sio kutumia kwenye mahitaji ya binafsi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Hai Elia Machange amewataka wajasiriamali waliopatiwa mikopo hiyo kulipa kwa wakati ili waweze kukidhi kupatiwa mikopo mingine pale watakapohitaji.
Machange amewahakikishia ushirikiano na usaidizi wa idara za halmashauri ikiwemo Idara ya Maendeleo ya Jamii hasa wakati wa kutekeleza miradi walioamua kuitekeleza.
Halmashauri ya Wilaya ya Hai ni miongoni mwa halmasahauri zinazotekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia kumi katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya Wanawake,Vijana na watu wenye Ulemavu na kwa mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri hiyo imetenga kiasi cha zaidi ya Sh. Million 176 kwa ajili ya kuwezesha makundi hayo.
Vikundi vilivyopatiwa Mkopo huo ni vikundi vya Wanawake 7,Vijana 4 na vikundi vya watu wenye wenye ulemavu vitatu ambapo vinajishughuisha na shuhuli mbalimbali za Kilimo na Ufugaji pamoja na viwanda vidogovidogo vya usindikaji ikiwemo mbogamboga na matunda.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai