Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amekabidhi mikopo inayotokana na asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri ya wilaya ya Hai yenye jumla ya shilingi Milioni 142 katika vikundi vya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu
Akikabidhi mikopo hiyo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amewataka wale wote waliopata mikopo kuzalisha ajira zaidi miongoni mwa wanakikundi na jamii kwa ujumla kama ilivyo adhima ya serikali.
Amesema kuwa vikundi hivyo ni vyema vikatambua kuwa fedha hizo si zawadi bali ni mkopo ulio na masharti nafuu kwa lengo la kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi.
"Ndugu zangu mnaopokea mikopo hii kila mara nasema mikopo hii sii zawadi bali ina masharti nafuu na hivyo tunapaswa kuzirejesha, na hapa naomba niwaambie hatutomfumbia macho ambaye hatafanya rejesho kwakuwa tukirejesha tunatoa fursa kwa vikundi vingine kuzidi kukopesheka". Alisema Saashisha Mafuwe.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Hai juu ya suala la utoaji wa mikopo hiyo, Mkuu wa wilaya ya Hai Amir Mkalipa amewaomba madiwani wa halmashauri hiyo kushirikiana na serikali katika kuhakikisha vikundi vinavyopata mikopo vinarejesha kwa wakati kwani madiwani hao ndio wanashiriki kwa hatua za awali za kuviidhinisha vikundi hivyo ili kupewa mikopo hiyo.
Mkalipa amesema kuwa mbali na jitihada zinazofanywa na madiwani, ofisi ya mkurugenzi na serikali kwa ujumla katika utoaji wa mikopo ni vyema kutambua kuwa kila mmoja anawajibu wa kuhakikisha fedha hizo za vikundi zinarejeshwa kwa wakati.
"Naombeni wote tutambue kuwa swala la vikundi kufanya marejesho kwa wakati ni ajenda yetu sote hapa ndani, sii agenda ya mkurugenzi pekee wala mbunge wala diwani ni ya kila mmoja wetu na mimi kama mkuu wa wilaya nitashirikiana nanyi nyote kuhakikisha vikundi hivi vinarejesha fedha hizo kwa wakati" Alisema Mkalipa.
Akizungumza katika makabidhiano hayo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mhe Edmund Rutaraka amewapongeza madiwani na wataalamu wa halmashauri kwa kusimamia vema na kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo za mikopo.
“Pesa hizi tunazo enda kutoa ni zao halmashauri ya wilaya ya Hai,maanake ni kwamba inatokana na asilimia kumi ya mapato yale ya ndani ambayo tumetenga kwa ajili ya vikundi vyetu vya akina mama,vijana na watu wenye ulemavu”
Awali akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo kwa vikundi hivyo, mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii Robert Mwanga amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 142 zimetolewa hii leo kwa vikundi 7 vya wanawake, vikundi 4 vya vijana na walemavu 3 ikiwa ni asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri ya wilaya ya Hai.
Miongoni mwa vifaa vilivuokabidhiwa kwa vikundi hivyo ni pamoja na pikipiki za magurudumu matatu (Guta), pikipiki za magurudumu mawili kwaajili ya kubebea abiria huku vikundi vingine vikiwa na miradi mingine kama vile usindikaji wa ndizi na parachichi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai