Jamii katika Wilaya ya Hai imetakiwa kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri ili kujitengenezea mazingira ya kujiimarisha kiuchumi na kuboresha hali ya maisha kwenye kaya na hatimaye taifa zima.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha za mkopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa mujibu wa sheria na kwamba halmashauri yake itahakikisha mikopo inatolewa kwa wahusika.
Akikabidhi shilingi milioni 53 kwa vikundi 11 kati yao vikundi vya wanawake 5 vimepewa shilingi 21,400,000 vikundi vya vijana 4 vimepewa shilingi 21,402,028 na vikundi 2 vya watu wenye ulemavu wamepatiwa shilingi 10,700,876; Sintoo amesema ni wajibu wa kila kikundi kureshesha fedha walizokopa ili ziweze kukopeshwa kwa vikundi vingine.
“Kila kikundi kinachoomba mkopo kitapatiwa; cha msingi wawe wamekidhi vigezo na matakwa ya kufaidika na mkopo huu.” Amesema Sintoo.
“Maafisa Maendeleo ya Jamii; muwaelimishe wananchi taratibu za kuomba mkopo lakini pia wale wanaokosa muwaambie sababu za wao kukosa mkopo ili kuondoa manung’uniko miongoni mwa jamii kwani kupata mkopo hakuzingatii aina yoyote ya upendeleo” Ameongeza.
Kwa upande mwingine Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella ameviasa vikundi vilivyopatiwa mkopo kutumia fedha hizo kutekeleza malengo waliyojiwekea hususani yale waliyotengenezea andiko lililofanya wapate mkopo huku akiwakumbusha kuzingatia mafunzo waliyopewa na wataalamu.
Wella amesema lengo la mkpo huo ni kuwainua wananchi kiuchumi hivyo matumizi sahihi ya fedha hizo yatachangia kutimia kwa lengo hilo la serikali inayofanya juhudi za kuelekea uchumi wa kati.
Naye Johnson Mushi mwenyekiti wa kikundi cha Mkombozi Albino walionufaika na mkopo huo kwa mara ya pili amesema kuwa walipewa mkopo mwaka juzi walioutumia kwenye kilimo cha viazi ambapo walipata faida na kuweza kureshesha mkopo vizuri na sasa wameomba tena ili kuongeza uzalishaji kwenye kilimo cha viazi na kuwashauri waombaji wengine kutumia fedha hizo kwa uaminifu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai