Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewataka wataalamu wa afya katika wilaya hiyo kutunza majengo na vifaa vya afya vinavyotumika kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na wataalamu wa afya kwenye hospitali ya wilaya hiyo Sintoo amesema kuwa serikali inatumia fedha nyingi kuweka miundombinu na kununua vifaa vya thamani ili kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya.
Amemtaka mratibu wa afya ya kinywa na meno kwenye hospitli hiyo kutunza jengo jipya la kitengo cha kinywa na meno pamoja na vifaa vilivyonunuliwa ili kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hoapitali ya Wilaya ya Hai Dkt. Ananoela Urassa amesema serikali kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri imejenga jengo jipya kwa shilingi milioni 84 kupanua huduma za kinywa na meno kwenye hospitali hiyo.
Pamoja na jengo hilo; Dkt. Urassa amesema kuwa serikali imenunua vifaa vya kisasa vya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na kiti maalumu cha kuhudumia wagonjwa wa meno chenye thamani ya shilingi milioni 47.
Naye Mratibu wa afya ya kinywa na meno kwenye hospitali ya wilaya ya Hai Dkt. Faridu akizungumzia vifaa vilivyonunuliwa amesema kuwa kitengo hicho kitatoa huduma bora kwa wananchi kwani vifaa vilivyonunuliwa ni vya kisasa na kwamba bado havipo kwenye hospitali nyingi nchini.
Amesema wamejipanga vizuri kutoa huduma bora kwa kutumia kiti chenye uwezo wa kutoa huduma Zaidi ya kumi kama kung’oa meno, kusafisha, kuziba, kusogeza na huduma nyingine kulingana na matakwa na tatizo alilonalo mgonjwa.
Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta ya afya ikiwa ni juhudi za kuwaletea wananchi huduma bora na kuwasogezea karibu kwa gharama nafuu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai