Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai amewaagiza Watendaji Kata na Vijiji katika halmashauri hiyo kuweka utaratibu wa kufuatilia na kutoa taarifa za watu wanaoingia kwenye maeneo yao ikiwa ni jitihada za kujikinga na ugonjwa wa Homa Kali ya mapafu wa Corona.
Sintoo ametoa maelekezo hayo pamoja na barua kwa watendaji wakati akipokea msaada wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu wa Corona wenye thamani ya Zaidi ya shilingi milioni moja wenye vifaa kama ndoo 17 za kunawia mikono pamoja na sabuni kutoka Taasisi ya Kijana Kwanza ya mkoani Kilimanjaro.
“Watendaji wa ngazi zote, hakikisheni hakuna mtu anayeingia kinyemela kwenye maeneo yenu; wekeni mtandao wa taarifa kwa kuwashirikisha mabalozi wa nyumba pamoja na wananchi kwa ujumla kuwapa taarifa ya wageni” amesema Sintoo.
Sintoo ameongeza kuwa Wilaya ya Hai ni moja kati ya wilaya zenye mwingiliano mkubwa wa watu hapa nchini ikichangiwa na uwepo wa kiwanja cha ndege, barabara kuu ya lami inayounganisha mikoa pamoja na kuwa karibu na mipaka ya nchi huku akiwashukuru wananchi ambao mara nyingi wamekuwa wakitoa taarifa juu ya watu wanaohisiwa kuingia nchini kinyemela wakikwepa maelekezo ya Serikali na kusema kuwa kufanya hivyo kunazidi kuonesha umakini walionao wananchi wa wilaya ya Hai.
Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Taasisi Kijana Kwanza Mujibu Idrisa amesema kuwa taasisi yao imeona ni vyema kutoa mchango wake wenye kuisaidia jamii kwa kupata ndoo za maji kwa ajili ya kila ofisi ya kata huku akiitaka jamii ione kuwa mapambano dhidi ya janga la CORONA yanapaswa kufanywa na kila mtu ili kuhakikisha maambukizi hayaendelei kusambaa.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Machame Magharibi Martini Munisi akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Hai amesema kuwa msaada huo unazidi kuonesha juhudi za makusudi kutoka katika taasisi mbalimbali za kupambana na Corona huku akiipongeza kamati Wilaya ya kupambana na ugonjwa huo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya akishirikiana na katibu wake Dkt. Irene Haule kwa kufanya kazi usiku na mchana na namna wanavyoshughulikia taarifa zinazotolewa na wananchi kuhusiana na mapambano ya ugonjwa huo.
Zoezi la kugawa vifaa hivyo ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa katika Wilaya ya Hai kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga, kuelekeza wafanya biashara na watoa huduma kuweka vifaa vya kunawia mikono kwenye maeneo yao, kuweka maji na sabuni kwenye mageti ya halmashauri na ofisi zilizo chini yake pamoja na vitakasa mikono kwenye milango ya kuingia ofisi za halmashauri
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai