Mkurugenzi Hai Awataka Watumishi Kushirikiana Kufanikisha Huduma Bora
Imetumwa: August 13th, 2021
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu huku akiwataka pia kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Myinga ameyasema hayo hii leo wakati akizungumza na watumishi wa makao makuu ya Wilaya lengo likiwa ni kujitambulisha kwao mara baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Amesema kuwa kipimo kikubwa katika utumishi wa umma ni matokeo mazuri ya kazi ambayo hupatikana kwa ushirikiano pamoja na mawasiliano mazuri ndani ya idara zote za Halmashauri.
"Tutapimana kutokana na matokeo ya vitu vinavyofanyika na hasa matokeo mazuri ya huduma kwa wananchi ikiwemo Afya, Elimu na huduma hizo zilete tija kwa wananchi na matokeo mazuri". Amesema Mkurugenzi Myinga.
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka watumishi wa halmashauri ya Hai kujikita katika ukusanyaji wa mapato jambo litakalopelekea halmashauri kuzidi kujiendesha kwa ufanisi pamoja na kupata hati safi.
Katika hatua nyingine Muyinga amesema kuwa hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wazembe na wabadhirifu wa mali za umma ili kuendelea kuimarisha uwajibikaji pamoja na kuleta ufanisi katika utumishi wa Umma huku pia akiwataka watumishi wote kuheshimiana na kutendeana haki ili kuleta mshikamano zaidi.
Hiki ni kikao cha kwanza Mkurugenzi Myinga kukutana na watumishi tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan takribani wiki mbili zilizopita.