Watumishi wa Umma wametakiwa kutekeleza majukumu waliyonayo kwa wananchi kwa kufanya kazi kwa bidi na kuzingatia sheria na taratibu za kazi.
Akiongea kwenye kikao cha kawaida cha watumishi; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema ni heshima kuajiriwa na Serikali hivyo watumishi wanatakiwa kufanya majukumu yao kwa uaminifu.
“Sisi tumebahatika kupata kazi; tujitahidi kile kidogo tunachopata tuhakikishe kinatumika kwenye matumizi sahihi” Amesema Sintoo.
Sintoo amewakumbusha watumishi kuhusu utaratibu wa watumishi kutoka nje ya eneo la kazi ikiwemo kusafiri kwenye wilaya na mikoa mingine.
Aidha, Sintoo amewataka watumishi kutumia ujuzi wa wataalamu wengine waliopo kwenye halmashauri katika kusaidiana katika shughuli za kujiongezea kipato kama kilimo na ufugaji ili kuwafanya watumishi wa umma kuishi maisha mazuri na familia zao.
Kwa upande wake Afisa Utumishi Augustina Kimbache ameelezea utaratibu unaowataka watumishi kujaza fomu za ruhusa wanapohitaji kwenda nje ya eneo la wilaya wanakofanyia kazi ili kuweka kumbukumbu na kfahamika mahali walipo.
“Utaratibu wa kuomba ruhusa unawahusu watumishi wote pamoja na wale wanaofanya kazi kwa mkataba wa muda maalumu kama kujitolea na wanafunzi wa mazoezi ambao wanafanya kazi chini ya Mkurugenzi Mtendaji” Ameongeza Kimbache.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Mwl. Julius Mduma amewasilisha shukrani za idara yake kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa namna alivyoendesha harambee maalumu ya kuboresha miundombinu ya shule ya Sekondari Mailisita.
Mduma amesema kuwa kiasi cha Shilingi milioni 65 zimepatikana kupitia michango ya wadau kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara pamoja na vyumba viwili vya madarasa kwenye shule hiyo.
Katika harambee hiyo Mkurugenzi Mtendaji ameahidi kujenga chumba kimoja cha darasa na samani zake vikiwa kwa ujumla na thamani ya shilingi milioni 25 ikiwa ni mchango wa halmashauri katika kuimarisha sekta ya elimu katika Wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ameweka utaratibu wa kukutana na watumishi wa idara na vitengo vyote wanaofanya kazi makao makuu ya halmashauri hiyo kila siku ya Jumatatu ili kufanya tathmini ya wiki iliyokwisha na kuweka mikakati ya utekelezaji wa kazi kwa wiki inayoanza.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai