Mkurugenzi Sintoo Ahimiza Matumizi Sahihi Fedha na Muda Kutekeleza Miradi ya Maendeleo
Imetumwa: February 15th, 2021
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amezitaka Idara za halmashauri hiyo zilizopokea fedha za miradi ya maendeleo kuelekeza nguvu katika kutekeleza miradi hiyo kwa wakati na kuhakikisha kuwa kazi inafanyika kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Akizungumza kwenye kikao cha asubuhi na watumishi wa makao makuu ya halmashauri hiyo Sintoo amesema kuwa fedha za Serikali hazitakiwi kukaa kwenye akaunti muda mrefu badala yake utekelezaji wa kazi za miradi uanze mara moja.
Sintoo amesema kuwa atafanya ziara za mara kwa mara kukagua utekelezaji wa miradi hiyo katika hatua zote kuanzia kazi inapoanza hadi inapofikia kukamilika akiambatana na wakuu wote wa idara na vitengo vya halmashauri yake huku akiahidi kufanya ziara ya kwanza tarehe 28 mwezi Machi.
Kwa upande mwingine Sintoo amewakumbusha watumishi wa Serikali kufanya kazi kwa moyo, kutumia vizuri rasilimali za serikali ikiwemo muda na kutekeleza majukumu waliyopangiwa kwa ufanisi huku wakihakikisha kuwa wananchi wanaohitaji huduma zao wanapata na kuridhika na huduma bora.
Ametumia kikao hicho kumpongeza Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Maria Kivelia kwa namna anavyosimamia watumishi ikiwemo barua alizowaandikia watendaji wa kata na vijiji kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Amewakumbusha watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha kuwa wanafanya vikao vya kisheria vya ngazi ya kata na halmashauri za vijiji ili kuwapa wananchi nafasi ya kufikisha mawazo yao katika utekelezaji wa majukumu.
Awali akitoa taarifa ya mapokezi ya fedha kutoka Serikali kuu Mkuu wa Idara ya Mipango Herick Marisham amesema kuwa halmashauri imepokea shilingi milioni mia mbili themanini (280,000,000) kati yake sh. 100,000,000 kwa ajili ya miradi ya afya na sh. 180,000,000 zitaelekezwa kwenye miradi ya elimu.
Marisham ameongeza kuwa fedha hizo zitapelekwa kwenye miradi ya ukamilishaji majengo ya maabara kwenye shule 6 za sekondari ndani ya halmashauri hiyo ambapo kila shule itapatiwa sh. 30,000,000.