Mkurugenzi Sintoo Aridhishwa Ukarabati Machinjio Wilayani Hai
Imetumwa: March 5th, 2021
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amekagua na kuridhishwa na ukarabati wa machinjio ya ng'ombe yaliyopo Mtaa wa Gezaulole Kata ya Bomang'ombe wilayani humo.
Sintoo ameeleza kuridhishwa na ukarabati huo mapema leo alipofika eneo hilo kwa ajili ya kukabidhiwa machinjio hayo na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Wilaya ya Hai ambaye ndiye aliyekuwa akisimamia ukarabati huo.
Sintoo amesema kuwa ukarabati huo ni wa awali ambao umetumia kiasi cha shilingi milioni 7 na kuwa bado halmashauri yake inao mpango wa kuiboresha zaidi ili iweze kukidhi mahitaji ya wilaya huku akielekeza eneo lote lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 10 ambalo ni sehemu ya machinjio hayo kufanyiwa usafi.
Pia Mkurugenzi huyo amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hai Noeli Nko kuwakamata na kuwachukulia hatua wale wote wanafanya biashara ya kuchinja ng'ombe kinyume na taratibu ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kwa mujibu wa sheria.
Awali akieleza changamoto ambazo zinazoikabili biashara hiyo, Nko amesema kuwa kumekuwa na mtindo wa baadhi ya wafanyabiashara kuchinja mifugo yao majumbani na kwenye mabucha nje ya utaratibu uliowekwa na serikali jambo ambalo ni hatari kwa afya ya walaji.
Hata hivyo amesema kuwa wataanza operesheni maalumu ya kupita katika mabucha na kufanya ukaguzi ili kubaini wale wote wanaouza kitoweo ambacho kimechinjwa kiholela.
Naye diwani wa Kata Bomang’ombe Mhe. Evod Njau amemuomba Mkurugenzi huyo kutenga kiasi cha fedha kwenye halmashauri yake kwa ajili ya kuunganisha umeme kwenye jengo hilo kwani wahudumu wa eneo hilo huwa wanatumia tochi kumulika kwa ajili yakufanya shughuli kutokana na machinjio hayo kuanza kufanya kazi saa tisa za usiku.
Ukarabati wa machinjio hayo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 7.5 ambapo fedha hizo ni kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.