Halmashauri ya Wilaya ya Hai imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyama vya ushirika ili kuvipa nafasi ya kushiriki ujenzi wa uchumi wa mtu mmojammoja na hatimaye kuchangia katika kuimarisha uchumi wa wilaya nzima.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa mwaka 2020 wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu (Hai Rural Teachers Saccos); Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema kuwa ofisi yake ipo tayari kushiriki katika kuimarisha chama hicho cha akiba na mikopo.
Amesema utayari huo unasababishwa na mafanikio yanayoonekana kwenye chama hicho ikiwemo kupata hati inayoridhisha kwa miaka minne mfululizo katika ukaguzi wa hesabu za chama, kufanikiwa kujenga jengo zuri la kisasa kuhudumia shughuli za chama pamoja na mwelekeo wa chama kujiendesha kwa faida.
Sintoo amewapongeza wananachama kwa mafanikio yaliyofikiwa na zaidi amepongeza viongozi wa chama hicho hususani bodi na menejimenti ya chama kwa namna wanavyosimamia chama kwa weledi na uaminifu.
Pia Sintoo amewataka watumishi wa umma wanaonufaika na huduma za chama hicho ikiwemo mikopo; kuitumia vizuri kujiimarisha kiuchumi kwa kufanya miradi ya kuwaingizia kipato na kuboresha maisha.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi; Mwenyekiti wa Bodi Terewandumi Swai amesema hadi kufikia 31/10/2020 chama kimeonesha ukuaji mkubwa ambapo akiba imeongezeka kutoka sh. 3,708,187,864 mwaka 2016 hadi kufikia 6,291,425,330.
Chama kimefanikiwa kutoa mikopo ya shilingi 41,513,612,000 tangu kianzishwe hadi mwisho wa mwezi Oktoba iliyosaidia wanachama kufanya shughuli za kilimo, ufugaji, ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, kununua vyombo vya usafiri na kuhudumia dharura mbalimbali.
Aidha chama kinaiomba serikali kuondoa tozo ya 2% ya makato ya inaolipwa hazina kila mwezi ambapo chama hutozwa shilingi milioni 6 kwa mwezi kwani chama kinaendelea kulipa kodi ya mapato na wanachama nao wanalipa kodi.
Hai Rural Teachers Saccos ni chama cha akiba na mikopo kinachohudumia watumishi wa umma katika wilaya za Hai na Siha kilichoanzishwa mwaka 2000 kikiwa na wanachama 67 waliokuwa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Hai wakiwa na mtaji wa shilingi 335,000 mwaka huu kikiwa kinatimiza miaka 20 na kwa ungozi wa bodi na Meneja Upendo Lyatuu chama kimefikisha wanachama 2,335 mwaka 2020 na kinaendelea kuvutia wanachama wapya.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai