Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewahakikishia walimu katika wilaya hiyo kuwa Serikali inawajali na itaendelea kuwapatia huduma wanazostahili ili kuimarisha utoaji elimu.
Akizungumza kwenye kikao kazi cha wataalamu wa elimu; Sintoo amesema kuwa Serikali itaendelea kuzipatia shule mahitaji ya kufanikisha mazingira mazuri ya kujifunza na ufundishaji bila kusahau kuwapatia walimu stahiki zao ikiwemo posho za madaraka kwa wakuu wa shule.
Aidha Sintoo amewataka waratibu elimu kata kutimiza kwa weledi na uaminifu mkubwa wajibu wao wa kusimamia shughuli za elimu kwenye shule zote zilizo katika kata zao ili kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa elimu kwa ubora unaotakiwa.
Pamoja na mambo mengine; Sintoo amepongeza hali ya ushirikiano unaooneshwa kwenye idara ya elimu na kusisitiza kuwa mafanikio katika mitihani ya ndani na ya kitaifa yatapatikana kwa kufanya kazi kwa ushirikiano.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Mwalimu Christopher Wangwe ametumia kikao kazi hicho kutoa shukrani kwa Rais John Magufuli na Serikali kwa namna inavyoboresha miundombinu na huduma za elimu na kuahidi kutekeleza wajibu wa kutunza miundombinu hiyo na kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
Kikao kazi hicho kilichoandaliwa Afisa elimu msingi kimewahusisha maafisa elimu taaluma, vifaa na takwimu, elimu ya watu wazima, afisa utumishi, Katibu wa TSC wilaya, waratibu elimu wa kata 17 pamoja na wakuu wa shule 131 za msingi za binafsi na za serikali katika wilaya ya Hai ili kuweka uelewa wa pamoja na kutembea pamoja kutekeleza wajibu wa kufikisha elimu kwa wanafunzi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai