MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt Anna Mghwira, ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria askari polisi wa kituo cha polisi cha Kia wilaya Hai wanaotuhumiwa kuwabugudhi wananchi wanaozunguka kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA)
Dkt. Mghwira amemwagiza kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro kuchunguza tuhuma za askari wa kituo hicho kufyatua risasi hewani kwenye makazi ya watu pamoja na kuwakimbiza watoto wa wafugaji waliokuwa katika malisho ya mifugo.
Aidha ameagiza kufanyike uchunguzi juu ya mkuu wa kituo cha Kia wa kwa nini hakuchukua hatua kwa askari wa kituo chake wanaotuhumiwa kwa utovu wa nidhamu kutokana na tukio lililotokea Aprili 7 mwaka huu.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sanya Stationi katika mkutano wa hadhara, Dkt Mghwira, amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro RPC Hamis Issa kuchunguza utendaji wa askari wa kituo hicho ambao umekuwa ukilalamikiwa na wanachi wa maeneo hayo.
Amesema tukio la askari hao kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwabugudhi wananchi linaleta taswira hasi kwamba serikali ndiyo inakandamiza wananchi wake na kususutiza umuhimu wa kudumisha amani na maelewano baina ya jamii zinazopakana kwenye eneo hilo.
“Askari tunawaheshimu sana; lakini pia ni sura ya serikali, sasa ikitokea askari amepiga mwananchi inaonekana kama serikali ndio imepiga mwananchi; hili naomba liangaliwe na lidhibitiwe vizuri” amesema Mghwira.
“Mimi sijamtuma mtu yeyote kuhusiana na suala lolote kuhusu KADCO hivi karibuni, na kama kuna anayesema nimemtuma, kama ni askari, Kamanda wa Polisi shughulika naye.”
Amesema kuwa serikali inatambua kuwa kuwa eneo hilo licha ya kuwa na uwanja wa ndege wa kimataifa pia wapo watu wanaoishi katika maeneo hayo na lazima waishi kwa amani wakati mgogoro wa msingi ukiendelea kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Amesema kuwa tatizo hilo pia linasababishwa na kutokuwepo kwa miundombinu ya kulishia mifugo na kutokwepo na mipaka imara itakayosaidia kuimarisha hali ya ulinzi kwenye maeneo yote na kuepusha migogoro hiyo.
Akizungumzia tukio hilo kijana Samweli Lazaro amesema siku ya tukio alikamtwa na askari na kukalishwa chini na kunyang’anywa silaha za jadi ambazo alikuwa nazo machungani.
“Walinikalisha chini na kunishikia bunduki na kuninyang’anya viatu na kuwafukuza watoto mpaka nyumbani na kupiga risasi mbili hewani” amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kia Yohana Laizer amesema kuwa tatizo kusumbuliwa na askari wa kituo cha KIA limekuwa sugu na limekuwa likitokea mara kwa mara na wakati mwingine hukamata mifugo na kuifungia kituoni.
“Tumechoka kufukuzwa na polisi kama wakimbizi, watoto wa shule wamekuwa wakikimbizwa na mbuzi zimekuwa zikifungiwa mahabusu kama watu, naomba utusaidie kuhusu suala hilo”amesema Diwani Laizer.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kuna hali ya kutoelewana kati ya wananchi wanaozunguka maeneo ya uwanja huo na kukiri kupokea malalamiko ya wananchi hao wakidai kunyanyaswa na polisi wa Kia.
“Mgogoro uliopo hapa ni ule wa KADCO na wananchi na polisi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kwa wananchi lakini hakuna kiongozi wa serikali aliyetuma kunyanyasa wananchi ”amesema Ole Sabaya
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC)Hamisi Issa amesema askari waliohusika na tukio hilo watachukuliwa hatua za kisheria wakibainika kufanya jambo hilo ambalo ni kinyume na taratibu za jeshi.
Aidha RPC Issa amewataka askari polisi katika mkoa wa Kilimanjaro kushirikiana kwa karibu na viongozi wa kijamii waliochaguliwa na wananchi ili kuimarisha mahusiano mazuri na kuimarisha ufanisi wa kazi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai