Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amewataka madereva na wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari kubwa katika kipindi hiki ambacho mvua kubwa za masika zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Babu ametoa rai hiyo katika kata ya Kia wilayani Hai alipofika majira ya asubuhi ya leo April 25, 2023 akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kujionea hali halisi ya mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo na maji kufunga barabara ya Moshi-Arusha.
Aidha mkuu huyo wa mkoa amemuagiza mkuu wa wilaya ya Hai Mhe. Amiri Mkalipa na kamati ya maafa ya wilaya kufika katika maeneo ya vijiji vya ukanda wa chini kujionea hali ilivyo kwa sasa kutokana na maji mengi kuelekea katika ukanda huo.
"Tumekuja kujionea hali halisi ya mafuriko ambayo yametokea hapa kwenye eneo hili la Kia, mvua kubwa ambazo zimenyesha jana huko milimani zimeteremsha maji mengi na kusababisha adha kubwa tangu alfajiri, magari kutoka Arusha na Moshi hayakuweza kupita"
"Nataka kutoa wito kwa madereva na kwa abiria ambao wapi kwenye magari kufuatia kipindi hiki kigumu sana cha mvua za masika wachukue tahadhari kubwa na tayari nimemwambia mkuu wa wilaya ya Hai Amiri Mkalipa yeye na kamati ya usalama na kamati ya maafa wasogee katika vijiji vya ukanda wa chini kufuatia taarifa yake kuwa maji yameanza kuingia kwenye nyumba za watu"
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Hai Mhe. Amiri Mkalipa wakati akielezea athari ya mvua hizo katika wilaya hiyo kwenye eneo la Kia kando ya barabara kuu ya Moshi-Arusha akaeleza kuwa hakuna madhara ya kibinadamu yaliyosabishwa na mafuriko hayo wilayani humo na badala yake maji yaliyojaa kwenye mashamba yanaweza kuathiri mazao yaliyopo mashambani.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai