Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Mhe. Amir Mkalipa ameagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa watu watakaobainika kuharibu vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti hususani kwenye vyanzo vya maji.
Mkalipa ambaye ameambatana na Katibu Tawala wilaya hiyo Upendo Wella, ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa bodi za maji wilaya ya Hai ikiwemo ya Uroki Bomang'ombe na Losaa Kia ambapo ameeleza kuwa waharibifu wa vyanzo vya maji wakiwemo wakataji wa miti wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Nimeagiza hatua kali zichukuliwe kwa wale watu ambao wanakata miti hasa kwenye vyanzo vya maji, mto Kikafu ndiyo watu wanakata miti na huko Machame watu wanavuna mbao, nimeagiza wachukuliwe hatua kali za kisheria na tutawaongezea adhabu ya mtu kupanda miti na lazima mti ukue, uumwagilie, ufanye nini lazima ukue"
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya tayari ameagiza wakala wa misitu wilaya hiyo TFS kutafuta miti rafiki ambayo itapandwa kwenye vyanzo vya maji vilivyopo wilayani Hai ikiwa ni programu maalum ya upandaji miti wilayani humo kwa lengo la kukabili mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha Mkalipa amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaochepusha maji kutoka kwenye miundombinu ya maji bila kufuata utaratibu kwani atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwa kupelekwa mahakamani pamoja na kusitishiwa huduma ya maji.
Awali akizungumza katika kikao hicho, meneja wa bodi ya maji Uroki Bomang'ombe Mhandisi Arnold Mbaruku amemueleza mkuu wa wilaya kuwa kwa sasa wana upungufu wa lita milioni 1 za maji kufuatia ukame uliosababisha kukauka kwa vyanzo vitatu vya maji na kuongeza kuwa mahitaji yao ya maji ni lita milioni 9 kwa siku.
Kwa upande wake meneja wa bodi ya maji Losaa Kia Jerry Joseph amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa anayoifanya hususan katika sekta ya maji na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili wananchi waendelee kunufaika na huduma nzuri ya maji safi na salama.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai