Mkuu wa Wilaya Awaasa Wakopaji Kutumia Fedha Kutimiza Mipango Waliyoombea Mkopo
Imetumwa: June 29th, 2021
"Tumieni fedha mlizopewa kwa malengo kudiwa na sii vinginevyo, kumekuwa na tabia ya kupata fedha hizi za mikopo na kisha mkienda huko mnaanza kupanga matumizi mengine ambayo mwisho wa siku mnaanza kukimbizana kwenye marejesho" DC HAI - Juma Irando.
Mkuu wa Wilaya ya Hai Juma Irando amewataka wananchi wa wilaya hiyo ambao wamepata fursa ya mikopo ya 10% ya mapato ya halmashauri kutumia fedha hizo kwa malengo kusudiwa ili kuwepo na tija katika kurejesha.
Irando ameyasema hayo wakati wa ugawaji wa mikopo hiyo yenye thamani ya shilingi milioni mia moja na tisa (109) kwa vikundi vipatavyo 17 ambavyo vimekidhi kupata mikopo hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema kuwa halmashauri yake itaendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa kushirikisha madiwani wake ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi wenye vikundi.
Aidha Sintoo amebainisha kuwa kwa kutumia wataalamu waliopo kwenye idara na vitengo; halmashauri hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu jinsi ya kujiunga, kuomba mikopo pamoja na namna sahihi ya kurejesha kwa wakati.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Bomang'ombe Evod Njau ameishukuru halmashauri kwa kutenga fedha hiyo huku pia akiviasa vikundi vya vijana wa bodaboda kutumia fursa hiyo na kujikwamua kiuchumi.
Amesema kuwa halmashauri imewashirikisha wao kama madiwani kuanzia ngazi za awali badala ya kuwashirikisha wakati wa kudai jambo ambalo lingewanyima uhuru wa kufuatilia maendeleo ya vikundi hivyo.