Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Amiri Mkalipa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi katika wilaya hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkalipa ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri wilaya hiyo DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amewataka watumishi kuwajibika kwa uwazi na uadilifu.
“Tumeona namna ambavyo Mhe. Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha nyingi kwenye wilaya yetu kwa ajili ya kusambaza maendeleo ya wananchi katika wilaya ya Hai ambapo jambo hili ni kubwa sana kwa hiyo tukawajibike kwa vitendo” amesema Mkalipa
“Twende tukawajibike, tuwe wawazi, waadilifu, wakweli, na kila aliyepewa dhamana ya kusaidia kwenye nafasi yake akatimize wajibu wake, tumeletwa hapa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan, tujipange kumsaidia vizuri kwa kuwahudumia wananchi wetu kwa misingi ya utawala bora iliyobeba haki na wajibu” ameongeza Mkalipa
Katibu tawala wilaya ya Hai Upendo Wella akizungumza katika kikao hicho cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo ametumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Amiri Mkalipa katika wilaya ya Hai ikiwa ni katika siku ya pili ya utekelezaji wa majukumu yake katika wilaya hiyo tangu alipoapishwa Februari 02, 2023.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Edmund Rutaraka amewataka wakuu wa taasisi za Serikali ikiwemo Ruwasa, Tarura na Tanesco kuhakikisha kuwa changamoto za wananchi zinazoibuliwa na madiwani zinatatuliwa kwa ufasaha na kwa wakati.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga ametumia kikao hicho kuwataka viongozi, watendaji wa halmashauri hiyo na wakuu wa taasisi mbalimbali kutumia kikamilifu redio Boma Hai fm kuwaeleza wananchi juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
“nawaasa kutumia redio yetu ya Boma Hai fm kwa matangazo mbalimbali, pamoja na kueleza miradi mbalimbali inayotekelezwa katika wilaya yetu, maendeleo makubwa yanaonekana Mhe. rais ametoa fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu ya madarasa, umeme, maji, barabara na kadhalika, vyote hivi tutumie redio Boma kuhabarisha umma na tutapita sawa kuwaambia kwenye vikao lakini redio hii lazima tuitumie kuwahabarisha wananchi hawa” amesema Myinga
Pamoja na mambo mengine kikao hicho cha kamati ya ushauri ya wilaya kimepitia rasimu ya bajeti 2023/2024 ya halmashauri hiyo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai