Wafanyabiashara wa sekta binafsi wametakiwa kulipa kodi kwa wakati ili kuepusha usumbufu na ucheleweshwaji wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya nchi jambo ambalo linamhusu kila mfanyabiashara katika ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Hai Juma Irando wakati wa uzinduzi wa baraza la wafanyabiashara wilaya ya Hai ambapo ameendelea kusisitiza suala la usafi wa mazingira kwa kila mtu wakati wa mkutano huo.
“mkutano huu unahusisha wafanyabiashara lakini wa sekta mbalimbali tujumuike kwa pamoja wakulipa kodi walipe kwa wakati , na wa ukarabati miundombinu wakarabati watu wanawekaje nyanya chini wapewe elimu ili wastaarabike huo ndo usafi” Amesema Irando.
Naye kaimu mkuu wa divisheni ya viwanda, biashara na uwekezaji Ernest Mhapa amesema dhumuni la kuanzisha baraza la biashara ngazi ya wilaya ni kukutanisha wafanyabiashara kutoka serikalini na sekta binafsi kujadiliana namna ya kuboresha mazingira ya biashara na namna ya kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.
Naye Afisa msimamizi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) upande wa kodi mkoa wa Kilimanjaro Odupoi Papaa amesema serikali imefuta ushuru wa vifungashio vya plastiki kwa mazao ya mboga mboga na maua na kuwataka wafanyabiashara kutumia vema fursa hiyo ili kukuza mitaji yao na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Papaa amesema kuwa eneo lingine lililofanyiwa marekebisho ni sheria ya magari ya kigeni (magari yanayobeba watalii) ambapo mwanzoni yalikua yanatozwa dola 16 sawa na shilingi 37,312 kwa gari moja na sasa imeshushwa mpaka dola 10 sawa na shilingi 23,320 kwa gari moja ili magari yaweze kuingia kwa wingi.
Ameongeza kuwa kwa kufanyia marekebisho sheria hizo imeifanya nchi ya Tanzania kuendana na jumuiya nyingine kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika uingizaji wa mapato ya nchi.
“sheria ya kodi ya mapato mfano wanaofanya biashara za mtandao muuzaji na mnunuzi wanauwezo wa kufanya biashara kwa njia ya mtandao kwa kuhakikisha mfanyabiashara analipa kodi bila hata kuwa na ofisi maalumu bali mtandao lakini kwa kufuata taratibu na sheria” Amesema Papaa
Akizungumzia suala la vizimba vya soko la walaji kwenye uzinduzi huo, Mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo Hai Zefania Gunda amesema hatua inayofuata kwenye swala la vizimba vilivyojengwa ni ukarabati ambao utawezesha bidhaa za wafanyabiashara hao kuonekana vizuri na pia kutawekwa mkondo wa kutolea maji taka ambayo yanatokana na bidhaa zikiwa zimenyeshewa katika hali ya kuhifadhi kwake.
Ameongeza kuwa elimu itaendelea kutolewa ili kufanya wafanyabiashara wafanye kazi zao vizuri na katika mazingira ya usafi kuanzia mpangilio wa maeneo ya stendi ndani ya bomang’ombe hadi maeneo ya sokoni.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai