Mkuu wa wilaya ya Hai Juma Irando ameiagiza ya halmashauri ya wilaya ya Hai kuitisha kikao na wafugaji mara kwa mara kwa lengo la kuwapatia elimu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kati ya wafugaji hao na wakulima hali itakayosaidia kuondoa migogoro isiyokuwa na tija baina yao.
Irando ametoa agizo hilo alipozungumza na wananchi wa wilaya hiyo January 12, 2023 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Sanya Station kilichopo kata ya Kia ambapo alimtaka mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika mara mara.
“Mkurugenzi pamoja na mwenyekiti wako wa halmashauri pamoja na viongozi wako, itisha kikao na wafugaji kila wakati muwe mnaitisha mikutano na wafugaji, ongeeni nao mjue changamoto zao waelekezeni wapeni elimu na namna nzuri ya kufuga lakini pia viongozi wote kuanzia ngazi ya kijiji, kata na kuendelea, tambueni mifugo yote iliyopo hapa katika wilaya yetu”
“Tunasema hivyo kwa sababu mipango bora ya matumizi ya ardhi haijafatwa, kwahiyo kaeni na viongozi hawa na wananchi mjadili pamoja na wakulima na wafugaji kuwa wapi kuwe na njia wapi kuwe na malisho wapi ni sehemu pekee ya kulima tu na wafugaji wasipitishe mifugo yao, sehemu ambayo tunasema ni ya wakulima tuache wakulima walime na sehemu ambayo ni ya malisho mkulima nae asiende kulima pale”
Aidha Irando amekemea tabia ya baadhi ya wafugaji kukaribisha mifugo kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya malisho huku akiwataka watendaji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuhakikisha wanadhibiti mifugo inayokaribishwa na baadhi ya watu wasiokuwa waamunifu hali inayosababisha usumbufu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuharibu mashamba.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Dionis Myinga ametaka watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha kuwa wananchi wanasomewa mapato na matumizi ya fedha wanazochanga kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwe na uwazi pamoja na ushirikishwaji kwani fedha ambazo wananchi wanachanga zinatakiwa zikafanye kazi iliyokusudiwa.
Kwa upande wake makamo wa mwenyekiti wa halmashauri hiyo Swalehe Swai amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa na utaratibu wa kuhudhuria kwa wingi mikutano ya hadhara inayoitishwa na viongozi kwani katika mikutano hutumika kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kutatuliwa kwa kero zao.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai