Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Hasan Bomboko, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mitatu ya maendeleo wilayani humo na kusisitiza kuwa hakuna changamoto ya kifedha, hivyo utekelezaji unapaswa kufanyika haraka
Miradi aliyotembelea ni Shule ya Sekondari Saasisha, Shule ya Wasichana Machame Girls, na Shule ya Sekondari Lemera, ambapo zaidi ya shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule hizo.
Katika hotuba yake, Mhe. Bomboko amewataka wakandarasi kuhakikisha wanakuwepo kwenye maeneo ya kazi na kuwa na nyaraka zote muhimu ili kuepusha ucheleweshaji wa miradi. "Fedha zipo, hatuna changamoto ya fedha. Mheshimiwa Rais ameleta fedha na zimeshawasili, sasa ni jukumu letu kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati," alisisitiza.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa kwa sasa si fedha, bali utekelezaji wa miradi katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Hai. Aliwataka viongozi wa idara husika kuhakikisha miradi inakamilika kwa mujibu wa mpango na viwango vilivyowekwa.
Aidha, Mhe. Bomboko amewaasa wananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila utulivu. "Tuendelee kumuombea Mheshimiwa Rais na viongozi wetu wote kwa afya njema, kwani maendeleo hayawezi kuja bila amani," amesema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai, Bwana Sospeter Magonera, ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Hai inafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa ufanisi.
Katibu Tawala amesema kuwa wakati mwingine halmashauri inalazimika kuwa na msisitizo mkubwa kwa wakandarasi na wasimamizi wa miradi ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa haraka na kwa kiwango kinachohitajika.
Hii inatokana na matarajio makubwa yaliyowekwa na Mheshimiwa Rais, ambaye anataka watoto wa Kitanzania wote kupata elimu bora katika mazingira bora.
Hivyo, fedha nyingi zinazotolewa kwa miradi ya elimu ni kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu ya kiwango cha juu, na kwa hiyo ni muhimu kuona miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango bora.
Ziara hii ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati, huku wananchi wakipata huduma bora zinazostahili.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai