*Bomboko azindua Wiki ya Maji kwa Kupanda Miti 500, Atoa Onyo kwa Wanaoharibu Vyanzo vya Maji*
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Hassan Mbomboko, amefanya uzinduzi wa Wiki ya Maji kwa kupanda miti zaidi ya 500 katika vyanzo vya maji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Bomboko ameeleza kuwa lengo kuu la maadhimisho haya ni kulinda vyanzo vya maji kwa kuhakikisha upandaji wa miti unafanyika kwa wingi. Amesisitiza kuwa kila kaya inapaswa kupanda miti kumi ili kufanikisha mpango wa kupanda zaidi ya miti milioni tano ifikapo mwaka 2030.
"Kaulimbiu ya Wiki ya Maji inalenga kulinda vyanzo vya maji kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho. Tumedhamiria kuhakikisha kuwa maji yanapatikana kwa kila mwananchi, kama ilivyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020," amesema.
Mheshimiwa Mbomboko ameufafanua kuwa kupitia serikali ya Mh! Rais Samia Suluhu Hassan, wilaya ya Hai imepokea zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya miradi ya maji, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa na miundombinu ya kusambaza maji kwa vijiji 11 vinavyohudumiwa na Mamlaka ya Maji ya Bomang'ombe.
Katika hatua ya kuhakikisha vyanzo vya maji vinabaki salama, Mheshimiwa Mbomboko ameagiza kuwa kila ofisi ya mamlaka ya maji inapaswa kuwa na banda maalum la upandaji miti. Pia, ameutoa onyo kali kwa wale wanaofanya shughuli za kibinafsi zinazoathiri vyanzo vya maji, akiwataka kuondoka mara moja.
"Natoa wito kwa wananchi wote kuwa walinzi wa vyanzo vya maji. Wale wanaofanya shughuli za kilimo, ufugaji au biashara katika maeneo ya vyanzo vya maji wanapaswa kuondoka mara moja. Nimewapa siku saba kuhakikisha wameondoka katika maeneo hayo," amesema.
Mwisho, ameagiza viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa ili kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai