Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ametangaza nia ya kujenga ukumbi wa mikutano kwa ajili ya matumizi ya jeshi la polisi wilayani humo.
Akizungumza mbele ya maafisa na askari katika viwanja vya polisi wilayani Hai Ole Sabaya amesema anachangia shilingi million tatu za kukarabati gari la polisi na kwamba kiasi cha shilingi million ishirini kitapatikana kwa ajili ya kujenga ukumbi wa mikutano.
Akikabidhi fedha taslimu kiasi cha shilingi million tatu za kuchangia kufanyia marekebisho gari la polisi kwa ajili ya matumizi ya jeshi hilo; Ole Sabaya amesema ofisi yake na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wataendelea kutatua changamoto zinazojitokeza ili kurahisisha utendaji wa jeshi hilo.
“Nakabidhi fedha hizi ili ziwasaidie kutatua changamoto yenu ya gari na mtambue kwamba serikali ipo pamoja nanyi na itashirikiana na jeshi kutatua changamoto zitakazojitokeza” amebainisha Ole Sabaya.
Aidha Ole Sabaya amewataka maafisa na askari polisi wa wilaya ya Hai kufanya kazi zao kwa weledi na kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi yao ili kuepuka malalamiko.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Katibu Tawala wilaya ya Hai Upendo Wella amewakumbusha maafisa na askari pamoja na watumishi wote wa umma katika wilaya ya Hai kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia miongozo ya kazi zao.
“Naendelea kusisitiza kwamba tuendelee kufanya kazi zetu kwa kuzingatia nidhamu na sheria zinazotuongoza kuhakikisha kuwa tunawatumikia wananchi kwa haki na usawa ili kutekeleza malengo makuu ya kuwahudumia vizuri wananchi wa wilaya ya Hai”. Amesema Wella.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amepongeza ushirikiano uliopo kati ya jeshi la polisi na ofisi yake kwa kufanya kazi pamoja na kwa karibu kwenye mambo yanayowakutanisha na kuomba ushirikiano huo kuendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa wilaya ya Hai.
Ole Sabaya ametumia hadhara hiyo kumtambulisha Brighton Mushi mdau wa maendeleo atakayeshirikiana naye kufanikisha azma ya kujenga ukumbi ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Hai anayefanya shughuli zake mkoani Arusha.
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Ole Sabaya amekuwa mstari wa mbele kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma katika wilaya yake kwa kuchangia miradi mbalimbali inayoibuliwa na wananchi pamoja na kununua pikipiki tatu na kukarabati nyingine tatu kwa jaili ya matumizi ya jeshi la polisi wilayani humo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai