Mwenyekiti wa Halmashauri Hai Aridhishwa Maandalizi Kupokea Kidato cha Kwanza Hai Sekondari
Imetumwa: January 6th, 2021
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambaye pia ni diwani wa kata ya Muungano Edmund Rutaraka amekagua hali ya mazingira ya shule ya sekondari Hai iliyopo katika kata hiyo kwa lengo la kubaini mapungufu yaliyopo ili yaweze kushughulikiwa na serikali kabla ya kupokea wanafunzi.
Rutaraka ameeleza kuridhishwa na hali ya shule hiyo hasa baada ya kujionea uwezo wake wa kuwapokea wanafunzi wote waliofaulu darasa la 7 na kupangiwa kujiunga na shule hiyo wakitoka katika shule za msingi zilizopo kata ya Muungano.
"Mimi kama diwani na pia mwenyekiti wa halnashauri ya wilaya ya Hai nimepita kujiridhisha kwa maelekezo yaliyokuwa yametolewa na mkurugenzi na kamati yake na kuzungumza na mkuu wa shule kuona wapi kuna upungufu ili baadaye tuweze kutekeleza kama serikali, lakini kwa maelezo na kwa hali niliyoiona kwenye shule hii idadi ya wanafunzi waliopangiwa mwanzoni 256 na hao wengine 180 wanaweza wakapokelewa kwenye shule hii ya Hai" amesema Rutaraka.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Warioba Alex ameeleza kufurahishwa na ujio wa mwenyekiti wa halmashauri shuleni hapo na ameiomba serikali kuanzisha shule nyingine itakayopokea wanafunzi wanaopata alama A pekee watakaokuwa wakikaa bweni kwani kwa sasa wanafunzi ambao wamekuwa wakipata alama hizo hupelekwa katika shule nyingine zilizopo nje ya wilaya.
"Kama ikiwezekana mtuletee mabweni lakini pia muanzishe shule ambazo wanafunzi watakuwa wanaingia wenye alama A tu na wakae bweni” Amesema Warioba.
Jumla ya wanafunzi 257 wamepangiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa awamu ya kwanza katika shule ya sekondari Hai na wanategemea kuanza masomo rasmi January 11, mwaka huu.