Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI George Kakunda amefurahishwa na kuridhishwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo Wilayani Hai na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji Yohana Sintoo kwa usimamizi mzuri inayoendana na thamani ya fedha iliyotumika.
Naibu Waziri alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake Wilayani humu ambapo alipata fursa ya kutembelea na kukagua upanuzi wa mradi wa maji wa Losaa-Kia pamoja na ujenzi wa mabweni katika shule ya Sekondari Harambee.
Pia amewapongeza wananchi kwa kuunga mkono juhudi za serikali kupitia michango ya fedha na nguvu kazi katika ujenzi wa bweni kwenye shule hiyo ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Shule hiyo ujenzi wa bweni hilo umegharimu kiasi cha shilingi 200,386,000/= ambapo kati ya hizo mchango wa wananchi ni shilingi 181,986,000/= michango iliyosimamiwa na serikali ya Kijiji na kuwataka wananchi wengine nchini kuiga mfano huo ili kuisaidia serikali kufikisha huduma muhimu kwa wananchi na kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.
Sambamba na pongezi hizo Kakunda ameitaka Halmashauri kutumia utaratibu wa ‘force account’ katika utekelezaji wa miradi midogo kwa kuwa uzoefu umeonyesha miradi mingi iliyofanyika kwa utaratibu huo imekamilika kwa wakati, kwa ubora huku ikipunguza gharama za utekelezaji wa miradi kwa kuwa mafundi wanaotumika ni mafundi eneo husika.
“Tumieni force account na tumieni mafundi wanaopatikana katika maeneo yenu kwani kazi zao zimekuwa bora kwenye maeneo mengi, mkifanya hivi mtakuwa mmetoa ajira kwa wananchi wenu lakini pia mtakuwa mmetekeleza miradi yenu kwa gharama nafuu” alisema Kakunda.
Kakunda pia amewataka walimu wa shule hiyo kufanya kazi kwa weledi na kufuata taratibu na sheria kwa kuwafundisha wanafunzi ipasavyo ili kuwawezesha kukua katika maadili yanayofaa ikiwa ni pamoja na ufaulu wa wanafunzi hao huku akiwahakikishia walimu kuwa serikali inatambua na kufanyia kazi madeni yao na kwamba hadi kufikia mwezi juni mwakani serikali itakuwa imelipa asilimia themanini ya madeni yanayodaiwa.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai