Naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Anjelina Mabula ameitaka idara ya ardhi Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, kutowafumbia macho wadaiwa sugu waliogoma au kuchelewa kulipia kodi ya ardhi wanazomiliki.
Ametoa wito huo wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Mara pamoja na kukagua mfumo wa ulipaji wa kodi ya ardhi katika halmashauri ili kuongeza kiwango cha ulipaji wa kodi.
Mabula amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya watu kumiliki viwanja huku wakikataa kuvipima na kuchukua hati jambo linaloleta migogoro mingi katika maeneo yao huku serikali ikipoteza kodi ya ardhi hivyo ni vema kufika mwisho wa kuwavumilia.
Mabula ameongeza kuwa Wizara ya ardhi inapoelekea katika bajeti itaenda kubadilisha baadhi ya taratibu ili kuweza kuvitambua viwanja ambavyo havijapimwa ili kubadilisha sheria na kuweka sheria itakayo mbana mmiliki kulipa na kuepuka wananchi kuibia serikali kodi, na kuondoa changamoto hiyo.
Aidha amesema kuwa wizara imejaribu kutoa vitendea kazi vitakavyosaidia kutunza kumbukumbu, kutambua wadaiwa na njia ya wao kufanya kazi kwa ufanisi, hivyo asingependa kusikia kuwa vitendea kazi hivyo vimeshindwa kufanyakazi kwa kutegemea wizara kukarabati au kuleta vipya, jambo ambalo ni kinyume kwani halmashauri ndio inayotakiwa kuendelea kuhudumia vifaa hivyo kwa kutenga fungu.
Awali akisoma ripoti ya utekelezaji wa ukusanyaji wa kodi ya ardhi kwa njia ya mfumo wa kisasa uliowekwa na Wizara; Kaimu Mkuu wa Idara ya ardhi Jacob Muhumba ametaja changamoto zilizopo za utumizi wa mfumo huo kufanyakazi taratibu sana kutokana na tatizo la mtandao.
Katika kutatua changamoto hiyo wamelazimika kutoa taarifa kwa katibu mkuu wizara ya ardhi hivyo kuamini kuwa changamoto hiyo itatatulika na kuendelea kutoa huduma hiyo kama ilivyokusudiwa.
Katika kuzungumzia migogoro ya ardhi ndani ya Wilaya ya Hai Jacob amesema kuwa migogoro ni ya kawaida huku mgogoro mkubwa ukiwa ni wa wananchi wa vijiji vya sanya station, Tindigani na Chemka kutokana na baadhi ya kaya katika vijiji hivyo kuingia katika eneo la uwanja wa Ndege jambo ambalo bado linashughulikiwa na ofisi ya waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai