Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili limeanza leo Ijumaa April 17 2020 kwa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga, Mara, SImiu,Mwanza, Shinyanga,Geita, Kagera,Kigoma na Tabora na linategemewa kufanyika kwa siku tatu hadi Jumapili April 19 2020.
Mkurugenzi Msaidizi wa elimu kwa Umma kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Rose Malo ameimbia Radio Boma Hai Fm iliyopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatekeleza takwa la kisheria linalowataka kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili katika kila uchaguzi mkuu na kuwa tayari awamu ya kwanza ilishafanyika mwaka jana na hivi sasa ni awamu ya pili inayoelekea katika uchaguzi mkuu mwezi Octobar mwaka huu.
Amesema kuwa zoezi hilo linahusisha kuwaandikisha wapiga kura wapya waliotimiza umri wa mika 18 au watakao timiza umri huo hadi Mwezi Octoba na pia kuboresha taarifa za wapiga kura ikiwa ni pamoja na wale ambao kadi zao zimeharibika, kupotea ama kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Pia amesema kuwa kutokana na uwepo wa Janga la Virusi vya Corona tume hiyo imeweka tahadhari zote katika vituo vyote vya kujiandikisha na kwamba kwa awamu hii uandikishaji unafanyika ndani ya kata na kila kata itakuwa na kituo kimoja kilichoteuliwa ambacho kitakuwa na vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na ndoo za maji na sabuni za kunawia mikono, vitakasa mikono na barako huku kukiwa na maelekezo ya wananchi kukaa kwa kupeana nafasi na kuzuia msongamano.
Aidha amewataka wananchi ambao wanatakiwa kushiriki zoezi hilo kufika vituoni na kuondoa hofu ya kupata maambukizi ya virusi hivyo kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi imehakikisha kuwa vituo vyote vimekidhi matakwa ya kiafya ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.
Uchaguzi Mkuu utafanyika mwezi Octoba mwaka huu ukihusiha kuchagua wawakilishi wa wananchi kwa ngazi ya Madiwani, Wabunge na Rais ikiwa ni jambo la muhimu katika nchi inayosimamia misingi ya demokrasia ambayo viongozi wake hupatikana kwa kuchaguliwa na kudumu madarakani kwa kipindi cha miaka mitano kwenye muhula mmoja.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai