NEMC Kaskazini Yahimiza Matumizi ya Vifungashio Vilivyothibitishwa
Imetumwa: June 22nd, 2021
Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za kutunza mazingira kwenye maeneo yao ili kuwa na mazingira rafiki kwa ustawi wa watu, mimea na wanyama.
Rai hiyo imetolewa na Mhandisi Nancy Nyenga wa NEMC Kanda ya Kaskazini wakati wa kuangamiza vifungashio vya plastiki vya kampuni ya Monsanto katika kiwanda cha Harsho kilichopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Akizungumzia vifungashio vya plastiki; Mhandisi Nyenga amesema kuwa jamii inatakiwa kuachana na matumizi ya vifungashio vilivyo chini ya kiwango kwani vinachangia kuharibu mazingira na watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya katazo la mifuko ya plastiki yam waka 2019.
“Kama mtu anatumia vifungashio ambavyo havina nembo ya TBS anatakiwa kuvisalimisha NEMC ili viangamizwe kwa utaratibu sahihi” Amesisitiza Nyenga.
Naye Joseph Lyakurwa wa kampuni ya Monsanto ya jijini Arusha amesema wameteketeza vifungashio walivyotumia awali kwa sababu ya kuwa chini ya kiwango cha ubora na kuanza kutumia vilivyo bora zaidi.
Lyakurwa amesisitiza kuwa kampuni ya Monsanto imejizatiti katika juhudi za kulinda mazingira na kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha utunzaji mazingira.
Kwa upande wake John Mushi; Meneja wa uteketezaji bidhaa amewakaribisha kampuni na taasisi zinazohitaji huduma yao kwa kuteketeza bidhaa za plastiki.
Akizungumzia utunzaji wa mazingira ; Afisa Mazingira wa wilaya ya Hai Alfred Njegite amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kutokomeza vifungashio visivyo na ubora kwa kuacha kutumia na kutoa taarifa ya wanaoviingiza nchini.