Vikundi vya utunzaji wa mazingira katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro vimeushukuru Wakala wa huduma za misitu hapa nchini TFS kwa kuvisaidia kupata mizinga ya ufugaji nyuki pamoja na mavazi ya kuvunia asali vitakavyosaidia kuongeza tija katika ufugaji nyuki.
Akizungumza baada ya kupokea mizinga hiyo katika kikundi cha Sifa Environmental Group Dominik Mmasy amesema kuwa ushirikiano uliooneshwa na idara ya misitu, nyuki pamoja na wakala wa huduma za misitu Tanzania ni wa kuigwa katika kuvisaidia vikundi hivyo kuzidi kukuwa zaidi kwani uwepo wa nyuki unasaidia kupunguza vitendo vya ukataji miti holela.
Awali akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa wakala wa huduma za misitu Tanzania wilaya ya Hai Evaline Mboya amesema wakala unatambua mchango wa vikundi hivyo katika utunzaji wa mazingira na ameahidi kuendelea kutoa vifaa mbalimbali kila mwaka vitakavyosaidia katika uhifadhi wa mazingira.
Naye Afisa Misitu Wilaya ya Hai Mbayani Molleli amesema vikundi vilivyopewa vifaa hivyo ni vile vilivyoonesha jitihada nzuri za kutunza na kuhifadhi mazingira huku akivitaka vikundi hivyo kuongeza juhudi katika utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake Afisa Nyuki Wilaya ya Hai Joyce Kombe amevitaka vikundi vilivyonufaika na vifaa hivyo kuvitumia katika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika mizinga ya nyuki ili kuongeza mazao ya asali na kujipatia kipato zaidi.
Vikundi vilivyonufaika ni pamoja na kikundi cha Sifa Environmental Group cha kijiji cha Kware, kikundi cha utunzaji mazingira Rundugai pamoja na kikundi cha Iroko kilichopo kata ya Weru weru.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai