Ofisi ya Waziri Mkuu Yawafuta Machozi Wahanga wa Mafuriko Wilaya ya Hai
Imetumwa: May 9th, 2021
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha kushughulikia maafa imetoa msaada wa vifaa kwa kaya zilizokumbwa na mafuriko katika kata za Weruweru, Masama Mashariki na Machame Magharibi wilaya ya Hai kutokana na mvua zilizosababisha mafuriko kati ya tarehe 21 na 22 mwezi April.
Msaada huo uliotolewa umehusisha vifaa kama magodoro 250, mablanketi 83, ndoo ndogo 167, sufuria 167, madumu ya maji 250, mikeka 1,666 na ndoo kubwa 67 ambavyo vitagawiwa kwa wahanga wa mafuriko katika Wilaya ya Hai.
Pamoja na msaada huo; wahanga hao wamepokea msaada mwingine kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Kaskazini Arusha ambayo imetoa tani 33 za mahindi kugawiwa kwa wahanga hao.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ametoa pole kwa wananchi waliofikiwa na maafa hayo huku pia akiishukuru Serikali kuu kwa msaada walioutoa.
Sabaya ametumia shughuli hiyo kutambua mchango wa wawakilishi wa wananchi akiwemo Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai na Diwani wa Kata ya Muungano Edmund Rutaraka kwa juhudi walizoonesha kuwatembelea wahanga na kushirikiana nao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema kwa sasa ofisi yake inaliratibu zoezi hilo kwa ukaribu na hadi kufikia mwishoni mwa wiki ijayo vifaa vilivyotolewa vitakuwa tayari vimewafikia walengwa.
Awali akisoma taarifa ya maafa mbele ya Mkuu wa wilaya ya Hai, Afisa Mazao Wilaya ya Hai Zefania Gunda kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo amesema kuwa kaya zilizokumbwa na mafuriko ni 543 na baada ya kufanyiwa tathimini imebainika kuwa zinazohitaji msaada wa dharura ni kaya 253 na 13 zikiachwa bila makazi baada ya kutokea kwa maafa hayo.
Maafa hayo yamesababishwa na mvua zilizonyesha ukanda wa juu wa Wilaya ya Hai usiku wa tarehe 21 kuamkia 22 mwezi Mei yaliyopelekea maporomoko ya maji yenye kasi kubwa na kusababisha madhara kwenye kata 10 za wilaya hiyo huku athari zaidi zikionekana kwenye kata za Weruweru, Masama Mashariki na Machame Magharibi.