Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amemshukuru Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi aliyoipeleka katika kila sekta ndani ya wilaya ya Hai.
Mbunge Saashisha ametoa shukrani hizo wakati akikabidhi mkopo wa vifaa (pikipiki) wenye thamani ya shilingi milioni 119 kwa vikundi vya vijana wanawake na watu wenye ulemavu ambapo mkopo huo unatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani yaa Halmashauri hiyo.
Ametoa rai kwa vijana waliopata mikopo ya pikipiki kuzitumia katika malengo yaliyokusudiwa na kuwataka kuwa mfano katika kuzingatia sheria za usalama barabarani.
"Hizi fedha zirejeshwe ili na wengine waweze kupata, lakini mmeambiwa hapa, ukilewa na zenyewe zinalewa (pikipiki), ukishindwa kufata sheria na pikipiki inashindwa kufata sheria, ninyi miili yenu siyo chuma, zingatieni sheria za usalama barabarani" amesema Saashisha.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amempongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na baraza la madiwani kwa usimamizi madhubuti wa mapato yanayopatikana ambapo pamoja na mambo mengine husaidia upatikanaji wa mikopo hiyo.
Aidha, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Hai Wang'uba Maganda ameeleza kuwa chama hicho kina Sera ya uchumi mzuri ulioimarika kwa ajili ya watu wake, ikiwa ni pamoja na wanawake vija na watu wenye ulemavu huku akiwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa weledi ili kujiimarisha kiuchumi.
Mikopo hiyo ya vifaa iliyohusisha pikipiki 34 imetolewa leo Julai 19, 2022 ikiwa ni agizo la kisheria linalozitaka halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani na kutoa mikopo hiyo kwa wananchi kwa lengo la kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo na kujinufaisha kiuchumi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai