Radio za Kijamii Kuongeza Nguvu Mapambano Dhidi ya Ukatili Kijinsia
Imetumwa: March 12th, 2021
Mtandao wa redio za kijamii Tanzania TADIO kwa kushirikiana na asasi isiyo ya kiserikali ya C Sema umetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 25 kutoka katika redio 10 za kijamii nchini ili kuziongezea uwezo katika mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake ikiwemo ukeketaji.
Radio Boma Hai fm inayomilikwa na Halmashauri ya wilaya ya Hai ni miongoni mwa redio zilizoshiriki mafunzo hayo ya siku 2 yaliyojikita kuweka mikakati ya kutumia redio za jamii kukabiliana na vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na wasichana nchini lengo likiwa ni kutokomeza ukeketaji pamoja na ndoa za utotoni.
Akizungumza katika mafunzo hayo, mdau wa mawasiliano na mahusiano ya jamii, Irene Makene amebainisha kuwa redio za jamii zina mchango mkubwa katika kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni kwa kuwa zipo karibu zaidi na jamii husika.
"Kwa sasa kumekuwa na ushirikishwaji mkubwa sana wa redio za kijamii na haya ni matokeo ya mtandao wa redio jamii TADIO ambao umezileta pamoja redio hizo na kuzitambulisha kwa wadau wa maendeleo na habari na kuona umuhimu wa kuzishirikisha hizi redio kwani zipo karibu zaidi na jamii ambayo haiwezi kupata habari kupitia vyombo vingine vya habari" amesema Irene Makene.
Awali akifungua mafunzo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya jiji la Arusha Angela Kiama, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao katika kukataa na kupinga ukatili dhidi ya watoto na wanawake huku akikiri kuwa wanahabari wana wigo mpana katika mapambano hayo.
Kwa upande wake Francis Selasini kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya NAFGEM amewataka wanahabari kuwa sehemu ya kuzuia ukatili kwa kufichua na kuripoti matukio hayo pindi yanapotendeka kwenye jamii ili kuondoa uwezekano wa wahusika kuachwa bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mikoa 6 imetajwa kuongoza katika matukio ya ukatili ikiwemo ukeketaji ni pamoja na Manyara, Arusha, Dodoma, Singida, Mara na Tanga.