Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kupata hati inayoridhisha kwenye ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2018/19.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wa Halmashauri hiyo; Dkt. Mghwira amesema ni jambo jema kuona halmashauri zikifanikiwa kufanya matumizi ya fedha za Serikali vizuri bila kuwa na ubadhirifu.
“Niwapongeze kwamafanikio mliyoyapata kwa kupata hati inayoridhisha kama ilivyoelezwa na Mtunza Hazina wa halmashauri yenu, hii inaonesha kuna juhudi za pamoja za madiwani, Mkurugenzi na wataalamu”
“Niwatie moyo ili kwenye ukaguzi ujao mpige hatua mbele na kupata hati safi ambayo mtaipata kwa kupunguza hoja zilizo kwenye uwezo wenu kuziondoa”
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amewataka watendaji wa halmashauri kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kwani ushirikiano huo utasaidia kuepuka kuzalisha hoja ambazo zinaweza kumalizwa ndani ya idara na vitengo vya halmashauri.
Aida Sabaya ameahidi mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa kazi za serikali zinazofanywa na halmashauri ili kuimarisha ufanisi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Helga Mchomvu amempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo Lengai Ole Sabaya kwa ushirikiano anaouonesha kwa baraza hilo na watumishi.
“Wanasema baniani mbaya kiatu chake dawa hivyo nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Hai kwa ushirikiano aliotuonesha na juhudi zake katika kuinua ukusanyaji wa mapato ya ndani. Tunashirikiana naye vizuri bila kujali tofauti ya kiitikadi” Amesema Mchomvu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai