Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Kassim Majaliwa amesema serikali imetekeleza na itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo katika wilaya ya Hai ikiwemo miradi ya Elimu, Afya, miundombinu ya barabara na Umeme.
Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt. John Magufuli, Saashisha Mafuwe mgombea ubunge wa jimbo la Hai na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji Cha kwasadala wilayani Hai.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. Magufuli katika wilaya ya Hai imefanikiwa kuboresha huduma za Afya ikiwa Ni pamoja na kutoa zaidi ya shilingi milioni 130 kwaajili ya ukarabati wa hospitali ya wilaya pamoja na kutoa sh. Bilioni 2.8 kwa ajili ya ununuzi wa dawa kwa kipindi cha miaka mitano.
Katika sekta ya maji Majaliwa amebainisha kuwa serikali imekwishatoa bilioni 520 kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa mradi wa maji kutoka Hai kwenda Arusha, shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha mradi wa maji LOSAA- KIA na zaidi ya shilingi milioni 700 zimetolewa kuimarisha skimu ya Machame Uroki.
Kwa upande wa Elimu amesema kuwa kwa miaka mitano serikali imekwishatoa zaidi ya Sh. Bilioni 2 kwa wilaya ya Hai kuendeleza mpango wa elimu bure na kwamba tayari imeanza kukarabati miundombinu ya shule zote zenye uhitaji huo.
Kuhusu Umeme amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na kwamba ametenga fedha zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo vijiji 5 kati ya 62 vilivyobaki katika wilaya ya Hai huku akibainisha kuwa gharama za kuunganishiwa umeme huo kwa wananchi ni sh. 27,000 tu.
Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai