Serikali Kuongeza Nguvu Kuboresha Barabara Wilayani Hai
Imetumwa: June 30th, 2021
Serikali imesema kuwa itaendelea kuzikarabati na kuzifanyia maboresho barabara mbalimbali za vijijini ili wananchi wake wazidi kupata huduma bora usafiri na kujikita zaidi katika shughuli za kimaendeleo ambapo imetenga kiasi mamilioni ya fedha kwaajili ya zoezi hilo.
Akijibu swali la mbunge wa Hai Saashisha Mafuwe, Naibu waziri wa TAMISEMI David Silinde amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 serikali ilitenga kiasi cha Shilingi Milioni 157.5 kwa ajili ya matengenezo madogomadogo ambapo pia kwa mwaka 2020/21 ilitenga shilingi milioni 189.35 kwa kuendelea kuzifanyia matengenezo barabara hizo, huku mwaka 2021/22 ikitenga kiasi cha Shilingi milioni 123.
Barabara hizo ni pamoja na barabara ya Kwasadala - Mashua yenye urefu wa Km 17, Shirinjoro - Mijongweni Km 4, Kalali - Nronga Km 5 na Sadala - Uswaa Km 9 ambapo hadi kufikia Agosti 21 mwaka huu matengenezo ya barabara hizo yatakuwa yamekamilika.
Katika swali la nyongeza Saashisha Mafuwe aliiomba pia serikali kuweka taa za barabarani katika maeneo ya Bomang'ombe, Machame na maeneo mengine ya mji ambayo yanakuwa kwa kasi na hayajawahi kuwekewa taa hizo tokea nchi ipate uhuru jambo ambalo serikali imepokea ombi hilo na kusema kwamba italifanyia kazi mapema iwezekanavyo.
Tangu aingie bungeni mwaka 2020 Mbunge wa Hai Saashisha Mafuwe barabara mbalimbali za jimbo la Hai zimeendelea kujengwa katika viwango mbalimbali ikiwemo changarawe na hata kwa kiwango cha Lami ikiwemo ile ya TTCL - RC Church iliyogharimu zaidi ya milion 300, barabara ya Dorcas na ile ya Rundugai ambapo ujenzi wake unaendelea hivi sasa.
Bunge limeahirishwa hii leo baada ya kukamilika kwa vikao vyake vya bajeti vilivyokaa kwa miezi mitatu, ambapo pia liliidhinisha bajeti ya Tsh trilion 36.6 kwa matumizi ya mwaka 2021/2022.