Serikali katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imetengua katazo la wananchi kutembea usiku katika Kijiji cha Isuki, Kata ya Masama Kati na kuagiza kupelekwa askari wa jeshi la polisi na jeshi la akiba kuimarisha ulinzi wa watu na mali zao.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kwenye Kijiji hicho Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amesema kuwa katazo la muda wa wananchi kutembea linatolewa kwa mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee.
“kwani ninyi mnaishi kwenye nchi yenu peke yenu? Niwaambie kwamba hakuna Jamhuri ya Isuki, na maamuzi ya kuzuia watu kutembea usiku nio jukumu la kijiji; hata mimi mkuu wa wilaya na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hatuwezi kutoa maamuzi hayo” amesema Sabaya.
Sabaya amesitisha shughuli zote za sungusungu wa kijiji hicho ambao kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa Kijiji Rabikira Makere wamekuwa wakiwakamata na kuwaadhibu wananchi walioonekana kutembea Zaidi ya saa mbili usiku na nafasi yao kuchukuliwa na askari wa jeshi la akiba.
Aidha Sabaya ameagiza TAKUKURU Wilaya ya Hai kuanzisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka kwa mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na baadhi ya wasaidizi wake wanaotuhumiwa kuhusika na unyanyasaji kwa wananchi.
Wakizungumza kwenye mkutano huo wakielezea madhila waliyopitia wakati wa kutekelezwa kwa katazo hilo baadhi ya wananchi wamesema kuwa wamekuwa wakikamatwa na sungusungu wa kijiji huku wakiadhibiwa kwa fimbo na faini ya mali au fedha taslimu.
Neeman Makere ni mmoja wa wanachi waliowahi kukutana na mkono wa sheria hiyo ya kijiji iliyotekelezwa kwake baada ya kutembea Zaidi ya muda ulioelekezwa na uongozi wa kijiji chao.
“Nilitoka kwa baba yangu wakanikamata wakaniingiza ndani ya ofisi nilipohoji kuhusu kosa langu na kutaka wanipeleke kituo cha polisi Bomang’ombe; mwenyekiti akawaambia wanitoe wanipeleke ‘goligota’ ndipo wakanitoa nje wakanifunga na pingu kwenye nguzo wakanichapa viboko 60 wakachukua elfu 30 na simu yenye thamani ya shilingi elfu 25”. Ameeleza Makere.
Naye Mtendaji wa Kijiji hicho Jared Swai amesema kuwa katika muhtasari wa vikao vya halmashauri ya kijiji hawakukubaliana uwepo wa sheria hiyo na ameshangazwa na adhabu zinazotolewa kwa wananchi hao bila utaratibu na kukiri kupokea malalamiko kutoka mwanchi ambae alikutana na tatizo hilo.
Swai amesema mbele ya Mkuu wa Wilaya kuwa amekuwa na wakati mgumu kutekeleza majukumu yake kutokana na tabia ya Mwenyekiti wa Kijiji kuhodhi madaraka na wakati mwingine kuingilia utendaji wa serikali kwa Imani kuwa yeye (mwenyekiti) ndiye sauti ya mwisho ya maamuzi kwenye kijiji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Rabikira Makere amesema kuwa adhabu hiyo ilipitishwa kwenye mkutano wa kijiji ikiwa ni jitihada za kukabiliana na matukio ya uhalifu ikiwemo wizi, ukabaji na hata matukio ya watu kuvamiwa na kuuawa yaliyokithiri kwenye kijiji chao.
Mkuu wa Wilaya amechukua maamuzi kuingilia mgogoro huo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi waliokuwa wakikandamizwa na sheria hiyo iliyowataka kutotembea zaidi ya saa mbili usiku na kwamba waliokamatwa waliadhibiwa kwa kufungwa pingu, kuchapwa fimbo 60, kulipa faini ya fedha kuanzia Sh. 30,000 hadi Sh. 80,000 au kupakwa upupu ‘washawasha’.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai