Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Juma Said Irando ameagiza kujengwa madarasa matatu katika shule ya msingi Nsongoro iliyopo kata ya Masama magharibi, kabla ya mwezi Januari mwaka 2022 baada ya shule hiyo kukumbwa na tetemeko la ardhi mwezi Novemba 2021.
Irando ametoa agizo hilo Nov 30 2021, alipotembelea na kukagua miundombinu ya shule hiyo kongwe ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru na kumtaka mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dionis Myinga kuhakikisha ujenzi huo unaanza mara moja kupitia fedha za mapato ya ndani.
“Nichukue fursa hii kukuelekeza mkurugenzi na bahati nzuri mkiti wa halmashauri naye yupo hapa, kupitia fedha zetu za maendeleo tuanze ujenzi wa madarasa matatu hapa katika shule hii tunafanya hivyo tukijua pia muda ni mfupi kwahiyo tuwe haraka katika hili, kwahiyo mkiti na mkurugenzi tuangalie katika mapato yetu ya ndani madarasa yajengwe hapa kabla ya mwezi wa kwanza” alisema DC Irando na kuongeza kuwa.
“Kwahiyo natumai hilo litakuwa limekidhi tatizo kubwa katika kijiji chetu cha Mashua na katika sherehe hizi za miaka 60 ya Uhuru tutakuwa tumeweka alama katika kijiji hiki cha Mashua, shule hii ni kongwe imeanzishwa mwaka 1960 inahitaji kujengwa upya uchakavu wake ni mkubwa wadau wote wa elimu tunawaomba pia muweze kushiriki kusaidia kutatua changamoto kubwa iliyopo katika shule hii”.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Edmund Rutaraka ameeleza kuwa pamoja na kuomba fedha kutoka Serikali kuu kwa ajili ya utatuzi wa changamoto ya miundombinu ya shule za msingi zilizopo wilaya ya Hai bado shule nyingi za msingi wilayani humo ni chakavu na zinahitaji kujengwa hivyo mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa wanaweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya shule hizo.
“Tumepanga kuanzia mwakani 2022 kupitia mapato yetu ya ndani tuweke kipaumbele kwenye kurekebisha hizi shule zetu, siyo Mashua tu hapa ndiyo mbovu shule karibia zote kwenye Halmashauri yetu mbovu”
Naye katibu tawala wilaya ya Hai Upendo Wella ametoa rai kwa wananchi kujitolea kwa kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa madarasa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai