Serikali katika Wilaya ya Hai imeazimia kusimamia upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wote wanaosoma katika shule za wilaya hiyo.
Msimamo huo wa serikali umetolewa mapema leo na Mkuu wa Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya alipofanya kikao na Wakuu wa Shule za Msingi kilichohudhuriwa pia na Wenyeviti wa Kamati za shule pamoja na wenyeviti wa vijiji zilipo shule hizo.
Sabaya amesema kuwa ni sharti wanafunzi wote wapatiwe chakula shuleni huku akiwasisitiza wazazi kuhakikisha kuwa wanawajibika kuchangia michango ya chakula na kwamba mzazi atakaeshindwa kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Sabaya amewakumbusha walimu kusimamia majukumu yao ya kufundisha na kuhakikisha wanafunzi wanaoletewa wanapata elimu wanayostahili, huku akiwakumbusha kamati za shule kutekeleza wajibu wao huku akiwasisitiza wazazi kuendelea na majukumu yao ya kuwapatia watoto mahitaji muhimu ikiwemo chakula, mavazi na daftari.
“Rais Magufuli anatoa shilingi bilioni 23.86 kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia elimu bure ambayo inatumika kulipa ada za wanafunzi, kuhudumia miundombinu, kuhudumia shughuli za utawala wa shule kwa kila mwanafunzi aliyeandikishwa kwenye shule husika ” Amesema Sabaya.
“Serikali inachofanya ni kuondoa zile gharama zinazofanya mwanafunzi kutokusoma kwa raha kwa kurudishwa nyumbani kwa ajili ya kwenda kuchukua michango inayohusiana na ukaaji wake shuleni ambayo ilikuwa ada, dharura, madawati na michango mingine iliyokuwepo”
Aidha Sabaya amezitaka kamati za shule na wenyeviti wa vijiji kuacha kuingilia majukumu ya kitaaluma yanayofanywa na ili kuwapa nafasi walimu kuwaandaa wanafunzi kwa namna inayotakiwa huku akihimiza umuhimu wa kuwa na mahusiano mazuri kati yao.
Nao walimu wakuu wa shule kwa umoja wao wamemuhakikishia mkuu wa wilaya kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidi kwa kuzingatia sheria na taratibu za elimu kuhakikisha kuwa wilaya ya Hai inaendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa ikiwemo Darasa la Saba na la Nne.
Kwa upande mwingine wenyeviti wa vijiji pamoja na wenyeviti wa kamati za shule wameahidi kutoa ushirikiano kwa walimu kwa kusimamia mambo yote yasiyohusu masuala ya taaluma ili kuwafanya walimu washughulikie malezi ya watoto kitaaluma na kuongeza ufaulu.
Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya akishirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wamejiwekea utaratibu wa kukutana na watumishi wa idara na vitengo vya halmashauri hiyo kila mwanzo wa mwaka kwa ajili ya kuweka mikakati ya utekelezaji wa kazi pamoja na kukutana mwisho wa mwaka kwa ajili ya kupima utekelezaji uliofanyika kitendo ambacho kimeongeza ufanisi wa watendaji kwenye halmashauri hiyo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai